CCM TANGA YASITISHA UJENZI WA SHULE SHIKIZI KUTOKANA NA KUJENGWA KATIKA CHANZO CHA MAJI

August 14, 2023









CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, kimesitisha ujezi wa shule shikizi inayojengwa katika  kijiji cha Mahezangulu, katika halmashauri ya Bumbuli, kutokana na shule hiyo kujengwa katika chanzo cha maji.


Akitoa maelekezo ya kusitishwa kwa ujenzi wa madarasa mawili ya shule hiyo inayojengwa katika kitongojo cha Kweusolo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdallah alisema wananchi lazima waheshimu vyanzo vya maji na utunzaji wa mazingira.


Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Mahezangulu, Seif Sekidele alisema kutokana na uhitaji wa shule shikizi kwa watoto wa kitongoji hicho walionelea wajenge shule katika eneo hilo licha ya kuwa ni eneo la chanzo cha maji kutokana na uhitaji mkubwa wa shule.


"Mheshimiwa Mwenyekiti kijiji chetu kina shule mbili za msingi lakini ukiingia shule ya Mahezangulu darasa lenye watoto 50 basi 32 wanatoka katika kitongoji hicho," alisema Mwenyekiti huyo wa kijiji.


Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Lushoto Erwin Sizinga, alisema serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 243 kwa ajili ya mradi wa maji wa kijiji hicho na eneo lililojengwa shule ni la chanzo cha maji cha mradi huo.

"Wenzetu wa bonde la mto Pangani walitwambia chanzo cha maji katika kijiji hiki kina maji ya kutosha isipokuwa wananchi wasilime katika chanzo hiki ili chanzo kiwe cha uhakika na endelevu," alisema Sezinga.

Mbunge wa jimbo la Bumbuli na Waziri wa Nishati, January Makamba, alisema alikataa kuwasaidia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo na kumweleza Mwenyekiti wa kijiji hicho kama mbunge yupo tayari kutoa fedha ili wapate eneo jingine kwa ajili ya kujenga shule nyingine badala ya hiyo.


Diwani wa kata ya Mahezangulu Rashid Abdallah 'Chid boy' alitaka serikali ikubali shule hiyo iendelee kujengwa katika eneo hilo na wataalamu watafute chanzo kingine cha maji ili watoto wa kitongoji hicho wapunguziwe umbali wa kwenda katika shule ya msingi Mahezangulu. 


Diwani alikubali kauli ya Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mahezangulu kwamba hakuna eneo jingine litakaloweza kujengwa shule zaidi ya eneo hilo ambalo ni la serikali ambalo zamani lilikuwa linepandwa miti na sasa ipo miti miwili tu na wananchi wanalima mahindi.

"Natoa maelekezo hapa pasiendelezwe paachwe, kuleta fedha kuindeleza shule hii ni kuendelea kuharibu chanzo cha maji bora tupate lawama kutoka kwa wananchi lakini tukilende hiki chanzo cha maji," alisema Mwenyekiti wa CCM mkoa.

Alimwagiza mkuu wa wilaya ya Lushoto Kalist Lazaro kuhakikisha wananchi hawalimi katika eneo hilo ili kuziokoa fedha za serikali zilizoletwa kwa ajili ya mradi wa maji, zisipotee bure.

Alisema CCM katika ilani yake ilisema kwamba hadi mwaka 2025 wananchi katika maeneo ya Vijiji watapata maji kwa asilimia 85 hivyo kuruhusu ujenzi huo kutasababisha ahadi hiyo isikamilike kwasababu ya watu kushindwa kutunza mazingira.

Mwenyekiti wa CCM mkoa ameendelea ziara zake za kutembelea wilaya za mkoa wa Tanga kuona uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya chama ya mwaka 2020-2025.

Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »