Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Tarehe 21 Apili 2018 atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kuongeza uwezo wa uhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika dhifa itakayofanyika kwenye viwanja vya Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula zilizopo Mtaa wa Kizota eneo la Viwanda Mjini Dodoma.
Mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani Milioni 55, ambao ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha Dola milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, mikataba ya ujenzi ilianza kutekelewa tarehe 9 Disemba 2017 ambapo Mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) huku msimamizi wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandashi wa habari na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba ameeleza kuwa Mradi huo utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa, ujenzi wa ofisi na kutekelezwa katika maeneo nane ambayo ni (Babati)-Manyara, Dodoma, Makambako-Njombe, Mbozi-Songwe, Shinyanga, Songea-Ruvuma, Sumbawanga-Rukwa na Mpanda-Katavi.
Baada ya mradi kukamilika Wakala utakuwa umeongeza uwezo wa kuhifahi kwa 250,000 MT zaidi (vihenge vya kisasa 190,000MT na maghala 60,000 MT) jambo ambalo litakuwa chachu na mafanikio yenye tija katika kuunga mkono Juhudi za utendaji wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.
Kupatikana kwa Mradi huo nchini ni jitihada za Serikali ambazo zitapelekea ukuaji wa uchumi nchini na kuchangia kuwezesha Tanzania ya viwanda ambapo kutawezesha maghala ya Wakala kuweza kuhifadhi akiba ya Chakula ambayo itaendana na mahitaji halisi ya dharura kulinganisha na ongezeko la watu nchini.
Hifadhi ya Chakula inayohitajika kukidhi mahitaji ya dharula kwa miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000 ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa inahitajika miaka ya 2008 Wakala ulipoanzishwa.
Aidha, Zikankuba alisema kuwa technolojia itakayotumika katika ujenzi wa vihenge vya kisasa, itawezesha Wakala kupunguza gharama za uendeshaji; kuhifadhi chakula kwa muda mrefu zaidi; kupunguza upotevu wa zao la mahindi baada ya kuvuna (posthaverst loss), kuongeza soko la mahindi nchini na kuimarisha usalama wa nafaka inayohifadhiwa kwa kudhibiti sumukuvu (Aflatoxin) kwa mahindi yaliyohifadhiwa. Jitihada hizi zinalenga katika kuimarisha uwezo wa Taifa katika kuimarisha usalama wa chakula nchini.