WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AKUTANA NA MKURUGENZI MTENDAJI MBADALA BENKI YA DUNIA, KANDA YA AFRIKA

April 19, 2018

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wakwanza kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe (hayumo pichani) kuhusu mpango kazi wa kuboresha uwekezaji Tanzania. Kushoto kwake ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga na Naibu Gavana anayeshughulikia Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila.

Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe (kulia) akimsikiliza kwa makini Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayumo pichani) wakati wa majadiliano ya namna ya kuendeleza miradi ya maendeleo nchini Tanzania, kushoto kwake ni Mshauri wa Mkurugenzi huyo Bw, Zarau Kibwe.
Picha ya pamoja ya wajumbe walioshiriki majadiliano ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe kuhusu uboreshaji wa sekta binafsi, miradi ya maendeleo, ukuaji wa uchumi pamoja na sekta ya ukuaji wa viwanda. Wanaopeana mikono kulia Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)kushoto Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe. Kutoka kulia ni Naibu Gavana anayeshughulikia Uchumi na Fedha Dkt. Yamungu Kayandabila, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Charles Kichere, wa pili kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga na wa pili kushoto ni Mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, kanda ya Afrika Bw, Zarau Kibwe.

Na. WFM- Washngton DC

Mikutano ya Bodi ya Magavana ya Shirika la Fedha la Kimataifa na kundi la Benki ya Dunia kwa mwaka 2018 imeanza rasmi mjini Washington D.C. Katika mikutano hiyo kutakuwa na Magavana, Mawaziri wa Fedha, Sekta Binafsi pamoja na Wanataaluma mbalimbali kuweza kujadili hali ya uchumi wa dunia pamoja na kupunguza umasikini.

Katika mikutano hiyo Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji Mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe, kuhusu maendeleo ya hali ya uchumi wa Tanzania huku akisisitiza kwamba ni wakati mzuri sasa wa kusemea hali ya uchumi wetu kwa nguvu zote.

Akiendelea kutoa ufafanuzi Dkt Mpango alieleza hatua ambazo Serikali imezifanya ili kuweka mazingira mazuri katika sekta binafsi, na kwamba Serikali imeandaa mpango kazi wa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika Taifa la Tanzania.

Pia Waziri Mpango alielezea miradi mikubwa ambayo nchi imeanza kuitekeleza, ikiwamo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa na Ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha Umeme wa Megawati 2100 la ‘Steigler's Gorge’ katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji.

Kupitia miradi hiyo ambayo Serikali imepanga kuifanikisha kwa wakati Dkt. Mpango alimuomba Bw. Bvumbe kuendelea kuzungumza na uongozi wa Benki ya Dunia ili uweze kutusaidia katika kuwezesha uwekeza katika miradi hiyo.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji mbadala Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika Bw. Andrew Bvumbe alisema kuwa anaipongeza Tanzania kwa jitihada inazozionesha hasa katika kupambana na rushwa na ametutia moyo tuendelee na juhudi zetu za kuimarisha uchumi wetu hususani katika sekta ya kilimo na pia amefurahishwa na hatua mbalimbali zinazofanya kwa ajili ya kuendeleza sekta ya viwanda.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha na Mipango

Washington D.C

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »