WAGONJWA 19,371 WATIBIWA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE KUTOKA JANUARI HADI MACHI 2018

April 19, 2018


Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha miezi mitatu ya Januari hadi Machi 2018 imeona jumla ya wagonjwa 19,371 wenye matatizo mbalimbali ya moyo kati ya hao wagonjwa wa nje ni 18,481 na waliolazwa ni 890.

Wagonjwa 105 walifanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua kati ya hao watu wazima 53 na watoto 52. Kati ya wagonjwa 105 waliofanyiwa upasuaji 66 walifanyiwa na madaktari wetu bingwa wa magonjwa ya moyo watoto wakiwa ni 35 na watu wazima 31.

Upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab ulifanyika kwa wagonjwa 231 kati ya hao watoto ni 20 na wakubwa 211. Kati ya wagonjwa 231 waliotibiwa wagonjwa watu wazima 211 walifanyiwa upasuaji na madaktari wetu wa ndani.

Kwa kipindi cha miezi mitatu tumekuwa na jumla ya kambi za matibabu nane (8) ambapo tulifanya matibabu kwa kushirikiana na washirika wetu kutoka nchi za Ujerumani, Israel, Australia , Marekani, India na Falme za Kiarabu. Katika kambi hizo jumla ya wagonjwa 39 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua kati ya hao watoto 17 na watu wazima 22. Wagonjwa 72 walifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kati ya hao watoto 20 na watu wazima 52.

Tumefanya upasuaji wa kuunganisha mishipa ya damu (AVF- Arterio Venous Fistula) kwa ajili ya kusafishia damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo (Hemodialysis) 36.

Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri hivyo basi tunawaomba wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara hii itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo au la na kama wanamatatizo wataweza kupata tiba kwa wakati.

Wazazi na walezi tunawaomba wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. Mtoto akianza kuuguwa magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha Hospitali na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulika mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo. Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo.

Aidha kwa upande wa gharama za matibabu Taasisi yetu imeyagawa katika makundi manne (4) tuna wagonjwa wanaotibiwa kwa bima mbalimbali ambazo tumeingia makataba nazo. Wagonjwa wanaolipia gharama zote wenyewe, wagonjwa wanaochangia kidogo huku gharama zingine zikilipwa na Serikali. Kundi la mwisho ni wagonjwa ambao hawalipii kabisa gharama za matibabu ikiwa watakidhi vigezo vyote vya kutokulipa.

Huduma zetu za matibabu ya moyo zinatolewa kwa watanzania wote wa Bara na Visiwani. Ifahamike kwamba fedha za matibabu zinazolipwa na wagonjwa zinatumika kununua vifaa tiba vya moyo kama mlango wa moyo (Valve), betri ya moyo (Pacemaker) na vinginevyo.

Kutokana na matibabu ya moyo kuwa ya gharama kubwa tunaendelea kuwasisitiza wananchi wajiunge na mifuko ya bima za afya ambayo itawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapohitaji kutibiwa. Pia itasaidia Hospitali yetu kuendelea kujiendesha yenyewe kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »