TANESCO TANGA YAWAPA TAHADHARI WANUNUZI WA NYUMBA

February 26, 2018
WANUNUZI wa nyumba na wapangaji mkoani Tanga wame tahadharishwa kuzikagua mita zao za umeme kabla ya kuishi ili kuepukana na kuingia gharama wasizotarajia wakati wa ukaguzi na wanaofanya ili kuwabaini wahujumu.
Tahadhari hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa Tanga Mhandisi Aloyce Shayo wakati akitolea ufafanuzi wa operesheni wanayoendelea nayo ili kuweza kubaini vitendo vya uhujumu
vinavyofanywa na wateja.

Alisema operesheni hiyo imekuwa ikilenga kukagua na kuangalia mita  na iwapo zinakutwa na makosa mbalimbali ikiwemo kuchezewa wanalazimika kusitisha huduma hiyo.

Aidha alisema kuwa operesheni inayoendelea Mkoani hapa ni ya kuwabaini wale wanaolihujumu Shirika kwa kuzichezea mita ambapo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa kulipa deni hilo kwa wakati kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kaimu Meneja huyo alisema wamegundua pia matatizo kwa baadhi ya wateja wao wanaponunua nyumba au kupangisha hawana utaratibu wa kuhakiki mita zao kupitia mafundi wao ili waweze kujiridhisha kama ziko salama badala yake wanasubiri mpaka wanapokuja kukaguliwa na kuadhibiwa.

Alisema hivi sasa ifike wakati wa jamii nzima kuelewa na kutekeleza wajibu wao wa kimsingi wa kuomba mafundi kutoka katika Shirika hilo kwa ajili ya ukaguzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo wanaohitaji kupangisha au kununua kabla ya kukutana na mkono wa sheria.

Hata hivyo alisema shirika hilo litaendelea na operesheni yake kwamkoa mzima na wale watakao bainika kuharibu miundombinu ya umeme sheria ziko wazi na kuongeza zoezi hilo ni endelevu ili kudhibiti uharibifu na uingiaji wa hasara kwa shirika usio tarajiwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »