Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (kushoto) akielezea mikakati ya usimamizi wa miradi ya umeme
nchini mbele ya Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Kampuni ya
Undelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) Wakandarasi wa Miradi ya Umeme
pamoja na Wasambazaji wa nyaya, tansfoma na nguzo (hawapo pichani)
Katikati ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo
na kulia ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi
Innocent Luoga
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu (kushoto) akifafanua jambo katika kikao hicho. Wengine kutoka
kulia ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi
Innocent Luoga, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana
Pallangyo na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Sehemu ya washiriki wa kikao hicho
wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani. (hayupo pichani).
………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha
linashughulikia haraka tatizo la kukatika kwa umeme katika mkoa wa
Mtwara ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kama
kawaida.
Waziri Kalemani alitoa agizo hilo
jana (tarehe 12 Oktoba, 2017) alipofanya kikao na Watendaji wa Wizara
ya Nishati, Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Kampuni ya
Undelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).
Wengine waliohudhuria kikao hicho
walikuwa ni pamoja na Naibu Waziri, Subira Mgalo, Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, Kaimu Kamishna wa Nishati na
Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga, wakandarasi wa miradi ya
usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na TANESCO na REA pamoja na
wasambazaji wa nyaya, nguzo na transfoma nchini.
Lengo la kikao hicho lilikuwa ni
kujitambulisha, kujadili namna ya kutekeleza miradi ya umeme nchini
pamoja na changamoto zake.
Alisema kumekuwepo na tatizo la
kutopatikana kwa umeme wa uhakika katika mkoa wa Mtwara ambapo ndio
chanzo cha gesi asilia inayotumika kuzalisha umeme.
Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika hilo, Dkt. Tito Mwinuka kuhakikisha unapatikana umeme wa dharura
kwa namna yoyote na kuongezwa katika mkoa wa Mtwara hivyo kumaliza
tatizo la kukatika kwa umeme kwa mara kwa mara.
Alisema mbali na kuweka umeme wa
dharura, shirika hilo linatakiwa kuhakikisha mitambo iliyoharibika
inakarabatiwa mapema ipasavyo na kuendelea na mchakato wa ununuzi wa
mitambo mipya kwa kasi kubwa ili hatimaye tatizo la umeme katika mkoa wa
Mtwara liwe historia.
“Wananchi wa Mtwara wanateseka
sana kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme la mara kwa mara
linaloukabili mkoa wao, ni jukumu la TANESCO kuhakikisha wananchi
wanapata umeme wa uhakika, na utekelezaji uanze mara moja,” alisema Dkt.
Kalemani.
Katika hatua nyingine, Waziri
Kalemani alisema kuwa Shirika la Tanesco linatarajiwa kuanzisha vituo
vidogo vidogo kwenye kata na tarafa ambavyo vitakuwa kwa ajili ya
kuunganishia wakazi umeme.
Alisema vituo hivyo vitakuwa rasmi
kwa ajili ya wateja kuhudumiwa kwa kukutana na watumishi wa Tanesco
moja kwa moja badala ya kukutana na vishoka wanaojifanya ni watumishi wa
Tanesco ambao huwatoza gharama kubwa na kuwalaghai.
Aidha aliwataka wananchi kufuata
taratibu za kuunganishiwa umeme kwa kuwa wameondoa ada ya maombi hivyo
wasiogope kuleta maombi wakidhani kuwa watatozwa bili yoyote.
Akielezea mikakati yake tangu
kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara Mpya ya Nishati, Dkt. Kalemani alisema
ameweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa umeme wa uhakika
unapatikana kwa gharama nafuu nchi nzima.
Alitaja mikakati hiyo kuwa ni
pamoja na kuhakikisha kuwa umeme unaozalishwa unafikia Megawati 5000
ifikapo mwaka 2020 ikiwemo ujenzi wa njia za kusafirisha umeme za
kilovolti 400 kwenye kanda zote nchini.
Wakati huohuo, Waziri Kalemani
aliwataka wakandarasi waliokabidhiwa miradi ya REA Awamu ya Tatu kuanza
kazi mara moja na kuhakikisha kuwa miradi inakamilika kwa wakati.
Naye Naibu Waziri wa Nishati,
Subira Mgalo alitoa pongezi wa serikali kujali watoa huduma wa ndani wa
usambazaji wa vifaa vya umeme kama vile nguzo, nyaya na transfoma na
kuwaomba kujikita kwenye uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini na
kuimarisha sekta ya viwanda nchini.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano
inaunga mkono uwekezaji wa viwanda ili kuhakikisha kuwa sekta ya
viwanda inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi na
kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
EmoticonEmoticon