Na mwandishi wetu, Zanzibar
Umoja
wa Wakulima wa Ndimu wa Kikundi cha Juhudi Zetu kilichopo Bwejuu, mjini
Unguja wametoa kilio chao cha kukosa soko la ndimu wanazozalisha kwa
uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Wakizungumza
na ugeni huo, wakulima hao wamesema kwa muda mrefu sasa wamekosa soko
la uhakika la mazao yao kwa kukosa mnunuzi wa uhakika licha ya kulima
kisasa na kupata mazao mengi.
Mmoja
wa wakulima hao Bw. Shafi Hamadi Mussa amesema kuwa kwa muda mrefu sasa
wamekosa soko la uhakika la mazao ya hali inayorudisha nyuma ari ya
kuendelea kulima zao hilo.
“Tunakatishwa tamaa kwa kukosa soko la uhakika licha uwekezaji mkubwa tunaoufanya katika kulima kisasa,” Bw. Mussa alisema.
Bw.
Mgana Khatibu Mgana, mkulima mwengine wa Umoja huo amesema changamoto ya
ukosefu wa masoko inaweza kutatuliwa kwa kupatiwa mkopo nafuu wa
kununulia mitambo ya uchakataji wa mazao ambayo itatumika kuongeza
thamani kwa mazao yao.
“Tunauomba
uongozi wa Benki ya Kilimo kutukopesha pesa za kununulia mitambo ya
kuchakata mazao yetu ili kuepuka adha ya ukosefu wa masoko wa mazao
haya,’ Bw. Mgana alisema.
Akijibu
kilio cha wakulima hao, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis
Assenga alisema Serikali imesikia kilio cha wakulima hao kwa kuanzisha
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na
mapungufu ya wakulima nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo
katika sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika kilimo nchini.
Aliongeza
kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa mazao
yote ya wakulima nchini kwa kuanzia na baadhi ya mazao ili kupata picha
halisi ya uhitaji wa rasilimali fedha kwa wakulima.
“Katika
hatua za awali, Benki imeainisha Minyororo Kumi na Nne (14) ya Ongezeko
la Thamani ya Bidhaa za Kilimo zitakayopewa kipaumbele katika kutoa
mikopo ni pamoja na Kilimo cha Nafaka (Mahindi na Mchele), Kilimo cha
Mazao ya Viwandani (Miwa na Korosho) na Ufugaji wa Ng’ombe (Ng’ombe wa
Nyama na Maziwa),” Bw. Assenga alisema.
Aliongeza
kuwa Benki inatoa mikopo kwa Kilimo cha Mbogamboga (Matunda, Mboga
Mboga na Viungo), Kilimo cha Mbegu za Mafuta ya Kupikia (Alizeti na
Ufuta) na kwa upande wa Kilimo cha Mazao ya Misitu ni Ufugaji wa Nyuki
na mazao yake.
Mengine ni Kilimo cha Ufugaji wa Kuku (Kuku wa Kienyeji na wa Kisasa) na Kilimo cha Samaki (Ufugaji wa Samaki).
Bw. Assenga aliwaahidi wakulima hao kuwa TADB itafanyia kazi maombi yao ili kuona namna ya haraka itakayotatua changamoto zao.
Zaidi
ya vipaumbele vilivyoainishwa, TADB pia imejipanga kusaidia minyororo
mingine ya ongezeko la thamani ya mazao ya Kilimo kwa utaratibu maalumu
kadiri ya upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na kusimamia uendeshaji
wa fedha mbalimbali zinazoelekezwa na Serikali ama wafadhili kwenye
Sekta ya Kilimo.
EmoticonEmoticon