WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATEMBELEA KIWANDA CHA KUUNGANISHA MATREKTA YA URSUS KILICHOPO KIBAHA. PIA ATEMBELEA ENO LA UWEKEZAJI LA KAMAL BAGAMOYO

May 24, 2017
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka benki mbalimbali nchini ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo kutoa mikopo kwa vikundi vya kilimo ili viweze kupata fedha za kununulia matrekta.

Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Sekta ya kilimo ili kwenda sambamba na adhma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Mei 23, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha kuunganisha Matrekta URSUS-TAMCO, Kibaha mkoani Pwani.

Amesema kiwanda hicho kinalenga kuboresha sekta ya kilimo nchini na kuongeza uzalishaji wa malighafi za viwandani kwa kuwa wakulima watakuwa na zana za kisasa.

Aidha, amevitaka vyuo vya kilimo nchini kununua matrekta hayo kwa lengo la kufundishia wanafunzi wake ili wanapohotimu wawe na uwezo wa kutumia zana hizo vizuri na kwenda kuwasaidia wakulima katika maeneo yao.

Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa Halmashauri nchini kuendelea kupanga matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya kilimo, uwekezaji, makazi, biashara na huduma za jamii, hivyo kuepuka migogoro ya ardhi kwa siku zijazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Bw. Mlingi Mkucha amesema wataunganisha matrekta 2,400,  harrow 2,400 na majembe 2,400 katika mradi huo wa kiwanda cha kuunganisha matrekta URSUS-TAMCO ikiwa ni mkataba wa awali.

Amesema kiwanda hicho kina wafanyakazi 27 kwa hatua za mwanzo. Aidha, idadi hiyo itaongezeka kutokana na mahitaji ambapo baadhi ya wafanyakazi watapewa mafunzo nchini Poland na watakaporudi watakuwa wakufunzi wa watakaoajiriwa.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa kiwanda hicho kimeazima wafanyakazi wengine wakiwemo watano kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 10 kutoka vyuo mbalimbali vya ufundi nchini, wawili kutoka CAMARTEC ambao wanashirikiana na wataalamu 10 kutoka URSUS kuunganisha matrekta.

Bw. Mkucha amesema wafanyakazi 10 kutoka Tanzania wanatarajiwa kwenda nchini Poland kufanya mafunzo mahsusi na watakaporejea watakuwa wakufunzi kwa watumishi wengine watakaoajiriwa katika kiwanda hicho.

Amesema mbali na ujenzi wa kiwanda hicho cha kuunganishia matrekta ya URSUS, mradi unahusisha uanzishwaji wa vituo vinane kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja na kuuzia matrekta, zana na vifaa vingine.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Everest Ndikilo amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda mkoani humo ni pamoja na kukatika kwa umeme, hivyo ameliomba Shirika la Umeme Tanzania (TANECO) kuongeza vituo vya kupozea umeme.

Awali Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage amesema kwa sasa nchini kuna viwanda vikubwa 393 kati yake 84 viko mkoani Pwani, ambapo amewaomba viongozi wa mkoa huo kutenga maeneo kwa ajili ya wanawake na vijana kuanzisha viwanda vidogo.

Mara baada ya kutembea kiwanda cha kuunganisha matrekta URSUS-TAMCO Waziri Mkuu alitembelea eneo la uwekezaji la Kamal (Kamal Indusrial Estate) lililoko katika Kata ya Kerege wilayani Bagamoyo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MEI 23,2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama moja kati ya mtrekta aina URSUS yanayounganishwa kwenye karakana ya TAMCO mjini Kibaha Mei 23, 2017.Kulia kwake ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akikagua matrekta aina ya URSUS yanayounganishwa katika karakana ya TAMCO mjini Kibaha Mei 23, 2017. Wengine pichani kutoka kulia kutoka kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NDC Mlingi Elisha Mkucha, Waziri wa Viwanda, Biahara na Uwekezaji, Charles Mwijage, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evaresti, Ndikilo na kulia kwake ni Mbunge wa Kibaha mjini Silvestry Koka.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama moja kati ya mtrekta aina URSUS yanayounganishwa kwenye karakana ya TAMCO mjini Kibaha Mei 23, 2017. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo akizungumza wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea eneo la uwekezaji la Kamal Industrial Estate lililopo Kerege Bagamoyo Mei 23, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka baada ya kutembelea eneo la uwekezaji la Kamal Industrual Estate lililopo Kerege, Bagamoyo Mei 23, 2017
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya viongozi, wabunge na wananchi waliohudhuria wakati alipotembelea eneo la uwekezaji la Kamal Industrial Estate lililopo Kerenge, Bagamoyo Mei 23, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya viongozi, wabunge na wananchi waliohudhuria wakati alipotembelea eneo la uwekezaji la Kamal Industrial Estate lililopo Kerenge, Bagamoyo Mei 23, 2017. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »