BALOZI WA UINGEREZA NCHINI TANZANIA AMTEMBELEA RC MAKONDA.

May 23, 2017


  Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda akimkaribisha mgeni wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. Sarah Cooke,alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar  na kufanya nae mazungumzo yenye lengo la kuongeza na kuimarisha Ushirikiano uliopo baina ya jiji la Dar es salaam na London, nchini Uingereza.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda akizungumza na mgeni wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. Sarah Cooke,alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. SARAH COOKE, amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe PAUL MAKONDA na kufanya nae mazungumzo yenye lengo la kuongeza na kuimarisha Ushirikiano uliopo baina ya jiji la Dar es salaam na London, nchini Uingereza.

Katika mazungumzo yao, Mhe MAKONDA na Bi. COOKE wamekubaliana kuongeza kasi ya Ushirikiano baina ya majiji makubwa mawili Dar es salaam Tanzania na London nchini Uingereza, makubaliano ambayo yatasaidia kupatikana kwa vifaa vya kisasa vya kuzuia na kupambana na majanga kama vile moto na mafuriko, ambapo Mhe MAKONDA ameomba kupatiwa magari ya kisasa ya shughuli za kuzima moto na uokoaji.

Mhe MAKONDA pia ameomba kusaidiwa vifaa maalum vya UTAMBUZ*I wa mifumo ya teknolojia ya kamera za kisasa zitakazofungwa *barabarani kwa ajili ya kusaidia USALAMA wa magari, raia na mali zao mifumo ambayo inafanya kazi katika jiji la London nchini Uingereza, hatua itakayokwenda sambamba na ujengewaji UWEZO kwa maofisa wa polisi wa Mkoa wa Dar es salaam katika matumizi ya mifumo hii.

Katika kukabiliana na changamoto ya MIGOGORO ya ARDHI mkoani Dar es salaam, Mhe MAKONDA ameomba kusaidiwa kuwajengea uwezo maafisa ARDHI na Mipango miji wa Mkoa wa Dar es salaam katika matumizi ya kisasa ya upimaji na upangaji ardhi, mafunzo ambayo yatakwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupima ardhi, jambo litakalosaidia kuondoa KERO ya upatikanaji wa HATI pamoja na vibali vya UJENZI Mkoa wa Dar es salaam.

Katika mazungumzo hayo, Mhe MAKONDA na Bi. COOKE wamejadili suala la uanzishwaji wa JIJI la FIKRA (brain storming center ) kwa ajili ya kuwakutanisha vijana wabunifu kama ilivyo kwa Tech City Uingereza.

Katika kuhitimisha mazungumzo yao, Mhe MAKONDA na Bi. COOKE kwa pamoja wamekubaliana kuzikutanisha timu za wataalamu kutoka London na Dar es salaam za kukabiliana na Majanga haraka iwezekanovyo.

Bi. COOKE, kwa upande  wake amefurahishwa na jinsi Mkuu wa Mkoa anavyopambana na vita ya dawa za kulevya ambayo imeathiri nguvu kazi kubwa sana katika jiji la Dar es salaam na kumuhakikishia kuwa Serikali ya Uingereza inaunga mkono jitihada zote zinazofanywa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam.

Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.

23/05/2017.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »