WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA UNUNUZI HISA ZA AWALI ZA VODACOM

April 14, 2017
Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Serikali imewataka watanzania kuchangamkia fursa ya ununuzi wa asilimia 25 ya hisa za awali za kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom zinazouzwa kwa watanzania pekee ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya fedha ya mwaka 2016 kwa lengo la kuwawezesha watanzania kuwa wamiliki makampuni ya simu za mikononi hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bi Beng’i Issa amesema hi ni fursa kubwa na muhimu kwa watanzania kuwa sehemu ya wamiliki wa makampuni ya simu za mikononi kupitia ununuzi wa hisa hizi za awali.

‘’Ni uwekezaji ambao ni salama sana na hauna hasara, kwa kuwa ukiwa hutaki kuendelea kuwa mwanahisa unauza hisa zako na kurudisha pesa zako na unaweza kupata faida’’.

Ununuzi wa hisa hizi utawawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa kampuni, watapata gawio la faida, wanaweza kutumia hisa kama dhamana za mikopo benki na wanaweza kuziuza hisa wanapokuwa na shida ya fedha.

Hisa hizi zinauzwa kwa mtanzania mmoja mmoja, watumishi walioajiriwa, wastaafu, makampuni yanayomilikiwa na watanzania, mashirika ya kitanzania, VICOBA, SACCOS, vikundi vya kijamii, wanawake na vijana. Aidha hisa moja inauzwa kwa shilling 850 na kiwango cha chini cha ununuzi ni hisa 100 na hakuna kikomo cha juu cha ununuzi wa hisa.

Baraza linatoa rai kwa Mashirika ya Hifadhi ya Jamii Nchini, Taasisi za fedha, Vikundi vya fedha vya kijamii kuwezesha wanachama na wateja wao kununua hisa hizi za awali.

Ununuzi wa Hisa hizi unapatikana kupitia matawi ya benki ya NBC, NMB, CRDB nchi nzima, mawakala wa soko la Hisa la Dar es Salaam, M-PESA na matawi mbali mbali ya benki za biashara nchini.

Baraza linawahamasisha watanzania wote kuchangamkia fursa hii muhimu ili kushiriki kikamilifu katika kumiliki uchumi wao na kufikia ndoto ya kuwa Taifa la uchumi wa kati kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Mwaka 2025.

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi linashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama radio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii kuhamasisha watanzania kunua hisa hizi za awali.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bw. Edward Kessy, akitoa ufafanuzi wa namna ya kununua hisa hizo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia kwa makini maelezo ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’I Issa (hayupo pichani) alipokuwa anatolea ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia kwa makini maelezo ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’I Issa (hayupo pichani) alipokuwa anatolea ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.(Piha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »