Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza baada ya sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Kichangani,
Magomeni jijini Dar es salaam Novemba 18, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Waislamu nchini waendelee kushirikiana na Serikali kulinda na
kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
Aidha, amewasihi waislam
kuimarisha umoja ,upendo ,mshimano miongoni mwao kwa kushirikiana na
jamii zinazowazunguka bila kujali tofauti zao za kiimani.
Ametoa wito huo leo mchana
(Ijumaa, Novemba 18, 2016) wakati akishiriki sala ya Ijumaa katika
msikiti wa Kichangani, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Amesema uwepo wa dini umewezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu hivyo kila mmoja ahakikishe suala hilo linaendelezwa.
Pia amewashauri waumini na
viongozi wa dini kuzingatia maadili ya dini ili kuepusha migongano isiyo
ya lazima hasa taasisi zinapokuwa na miradi.
Waziri Mkuu alitolea mfano
msikiti huo wa Kichangani chini ya Sheikh Walid umeweza kusuluhisha
hitilafu wenyewe bila kukimbilia Serikalini au mahakamani kusuluhishwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amesema Waislamu wana jukumu la kuwafunza elimu ya dini watoto wao na
kuhakikisha wanakua kwenye imani na kujengeka katika maadili mema.
Amesema dini inajenga maadili
mema kwa mtoto na kumwezesha kukua katika misingi ya uvumilivu na
inamuwezesha kumtambua Mwenyezi Mungu.
“Nimefarijika kuona vijana wengi
wameshiriki katika sala hii ya Ijumaa. Nawaomba wazazi waendelee
kuelimisha watoto umuhimu wa kufanya ibada,” amesema.
“Tuendelee kuwafundisha vijana
wetu umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kidini ili
wakikua waweze kuiendeleza kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Waziri Mkuu amewaomba waumini hao
waendelee kuwaombea viongozi wa kitaifa ili waweze kutekeleza vizuri
majukumu yao na kufikia malengo yanayotarajiwa na wananchi.
EmoticonEmoticon