SERIKALI KUENDELEA KULINDA KAZI ZA WASANII NCHINI

April 19, 2016

FIS1
Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa kodi toka Mamlaka ya Mapato    Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo akionesha kwa waandishi wa Habari leo Jijini Dar es salaam moja ya CD zilizokamatwa wakati wa msako wa kubaini wale wote wanaojihusisha na uuzaji na usambazaji wa kazi za wasanii bila kuwa na stempu za kodi katika bidhaa za filamu na muziki. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce Fissoo na mwisho kulia ni Afisa Habari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bi Mariam Mwayera.
FIS2
Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa kodi toka Mamlaka ya Mapato    Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo (katikati) akitoa wito leo Jijini Dar es salaam  kwa wasambazaji na wauzaji wa kazi za Filamu na muziki kuzingatia sheria na Kanuni zinazosimamia sekta hiyo kwa kuwa Serikali itawachukulia hatua kali wale wote watakaoenda kinyume cha sheria na taratibu zilizopo ikiwemo kutozwa faini isiyopungua milioni tano au kifungo kisichopungua miaka mitatu jela. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce Fissoo,Kushoto ni Afisa Utamaduni wa Bodi ya filamu Bw. Wilhadi Tairo.
FIS3
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce Fissoo akifafanua kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu mikakati ya Bodi hiyo kuhakiksha kuwa kazi za wasanii wa filamu zinaendana na maadili ya Taifa.kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Richard Kayombo.
FIS4
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Filamu Tanzania ukilenga kueleza Mikakati ya Serikali katika kulinda haki za wasanii wa filamu na Muziki zinalindwa.
( Picha na Frank Mvungi- Maelezo)
……………………………………………………………………………………………………………..
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeahidi kuendeleza msako wa wafanyabiashara wote wanaouza kazi za filamu na muziki bila kubandikwa stempu halali za kodi ili kuzilinda kazi hizo kwa ajili ya kuwanufaisha wasanii na kuhakikisha Serikali inapata mapato yake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma kwa Mlipa Kodi kutoka TRA Richard Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Kayombo amesema TRA kwa kushirikiana na wadau wa tasnia ya muziki na filamu imedhamiria kuhakikisha kuwa bidhaa za filamu na muziki zenye stempu za kodi ndizo zinazoingizwa sokoni ili kulinda kazi za wasanii wa taifa letu dhidi ya dhuluma zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.
“Msako huu endelevu utahusisha kukamata bidhaa zote ambazo hazijabandikwa stempu za kodi na kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa sheria.” Alieleza Kayombo.
Aidha Kayombo amefafanua kuwa kwa kipindi cha mwezi Februari na Machi 2016, TRA kwa kushirikiana na Dalali wa Mahakama Yono Auction Mart & Company Limited ilifanya msako jijini Dar es Salaam na kukamata jumla ya CD na DVD zenye thamani zaidi ya shilingi Bilioni 1.3 ambazo zilisambazwa bila kufuata sheria hivyo kukwepa kodi ya ushuru ipatayo shilingi Milioni 31.9 na gharama za stempu zaidi ya shilingi Milioni 11.1.
TRA inawatahadharisha wale wote wanaosambaza na kuuza kazi za filamu na muziki ambazo hazijabandikwa stempu kuacha mara moja na kufuata utaratibu wa kupata stempu hizo katika ofisi za TRA ili wawe na uhalali wa kuuza bidhaa hizo kinyume chake hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »