Droo ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation
Cup) imefanyika usiku huu moja kwa moja (live) kupitia kituo cha
luninga cha AzamTwo, huku timu za Coastal Union na Mwadui FC zikipata
nafasi ya kucheza nyumbani.
Katika droo hiyo iliyochezeshwa na mchezaji mstaafu wa timu ya timu
ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Esther Chaburuma, imewashuhudia
vigogo wa Ligi Kuu ya Vodacom, Azam FC na Young Africans wakipata nafasi
ya kucheza michezo hiyo katika viwanja vya ugenini.
Mwadui FC watakua wenyeji wa Azam FC katika mchezo unaotarajiwa
kucheza Aprili 24, 2016 mjini Shinyanga, huku wagosi wa Kaya Coastal
Union wakicheza dhidi ya Young Africans katika uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga siku hiyo hiyo.
Washindi wa michezo hiyo ya Nusu Fainali, watakutana fainali ya kombe
hilo itakayofanyika mwezi Mei, ambapo Bingwa wake ataiwakilisha
Tanzania katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).
Wakati huo huo wadhamini wa michuano hiyo Azamtv kupitia kituo chake
cha michezo cha Azam Sports, leo wameweza kulionyesha hadharani kwa mara
ya kwanza kombe la ubingwa kukikabidhi kwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa
Selestine.