Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akisalimiana na
Brigedi Kamanda wa 101 KV Zanzibar, Brigadia Jenerali, Cylir Mhaiki,
kabla ya kufanya mazungumzo na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama
mjini Zanzibar. Kulia ni Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokozi,
Zanzibar, Ali Abdalla Maalimmosi. Waziri Kitwanga yupo Zanzibar kwa kwa
ziara ya kikazi ya kuangalia hali ya uimarishaji wa usalama visiwani
humo.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (katikati) akizungumza na
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mjini Zanzibar. Waziri Kitwanga
aliwataka wakuu hao kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unazidi
kuimarishwa katika maeneo mbalimbali ya visiwani humo. Kikao hicho
kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jeshi la Zimamoto na Uokozi
mjini humo.
Brigedi
Kamanda wa 101 KV Zanzibar, Brigadia Jenerali, Cylir Mhaiki (kulia)
akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
(katikati) wakati wa kikao cha Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama
mjini Zanzibar na Waziri huyo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano
wa Jeshi la Zimamoto na Uokozi, Zanzibar.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kulia) akizungumza na
waandishi wa habari mjini Zanzibar mara baada ya kumaliza mazungumzo na
Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama visiwani humo. Waziri Kitwanga
amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi Machi 20, 2016
bila kutishwa na mtu yeyote, na kila mwananchi aondoe hofu siku hiyo
kwani vyombo vya ulinzi vimejipanga vizuri kwa ajili ya kuusimamia
uchaguzi huo.
Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
…………………………………………………………………………………………
Na Felix Mwagara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka
wananchi wa visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi Machi 20, 2016 ili
waweze kupiga kura kwa amani na utulivu bila kubughudhiwa na mtu yeyote.
Kitwanga amesema kuwa ulinzi umeimarishwa na kuwataka wananchi
visiwani humo kujitokeza kwa wingi kuja kumchagua kiongozi wanaompenda
siku ya uchaguzi huo na watarejea nyumbani kwao salama mara baada ya
kumaliza kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza
mazungumzo na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya
Polisi Zanzibar na baadaye kuzungumza na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na
Usalama, Waziri Kitwanga alisisitiza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama
vimejiandaa vizuri na wananchi waondoe shaka kwani hawatakubali vurugu
ya aina yoyote itokee.
“Jitokezeni kupiga kura siku ya uchaguzi kwani ni haki yenu,
nawahakikishia usalama upo na wa hali ya juu, asijitokeze mtu yeyote
akawatisha kutokuja kupiga kura, tumejipanga vizuri na lengo letu kubwa
kabisa ni kuwalinda wananchi,” alisema Kitwanga.
Hata hivyo Waziri Kitwanga alisema hakuna mwananchi yeyote
anayehama kwakuogopa vurugu siku ya uchaguzi bali watu wanasafiri
kwasababu mbalimbali ikiwemo hiki ni kipindi cha maandalizi ya Sikukuu
ya Pasaka, baadhi ya wananchi wanaenda kula sikukuu maeneo mbalimbali
nchini na wengine wanasafiri kutokana na majukumu mbalimbali na sio
wamekuwa wakimbizi wakikimbia sehemu zao kama inavyoenezwa.
“Acheni kusikia habari za mitaani amani ipo, jitokezi kupiga
kura na hii habari mnayosikia eti watu wameanza kuyakimbia makazi yao ni
uzushi tu, hakuna kitu kama hicho, wananchi wanaendelea na shughuli
zako kama kawaida na vyombo vya ulinzi vimejipanga kwa ajili ya kulinda
usalama wa raia na mali zao,” alisema Kitwanga.
Waziri Kitwanga amewasili Zanzibar leo kwa ajili ya ziara ya
kikazi ya kuimarisha usalama zaidi visiwani humo pamoja na kujua
mikakati iliyowekwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu usimamizi wa
uchaguzi huo.