Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanznaia (TFF), Jamal Malinzi
amempongeza Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwa kukubali uteuzi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) na GAVI utakaomfanya
kuwa bingwa wa chanjo na balozi wa mradi wa Africa United Duniani.
“Familia ya mpira wa miguu inajua umuhimu wa chanjo na hasa katika
maendeleo ya vipaji na wanamichezo kwa ujumla na jinisi chanjo
inavyoweza kuwapa watoto siyo tu fursa ya maendeleo bali pia haki ya
kuishi” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Rais wa TFF, Jamal
Malinzi.
Katika barua hiyo, Malinzi ameelezea furaha ya TFF kuona kiongozi wa
Tanzania akiongoza mapambano ya kuokoa afya na uhai wa kizazi cha sasa
na kijacho katika Afrika na dunia kwa ujumla.
“TFF itaunga mkono juhudi zako ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na
ushirika wa chanjo” ilimalizia barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa
kwa Rais wa Caf, Issa Hayatou.