Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara mzunguko wa 17 unatarajiwa
kuendelea kesho Jumatano kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja
mbalimbali, huku kila timu ikisaka pointi tatu muhimu kwenye msimamo wa
ligi hiyo.
Kesho Jumatano, Simba SC watakua wenyeji wa maafande wa Mgambo
Shooting kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, JKT Ruvu
watawakaribisha Mbeya City katika uwanja wa kumbukumu ya Karume Ilala,
huku Mtibwa Sugar wakicheza dhidi ya Toto Africans katika uwanja wa
Manungu – Turiani.
Jijini Mbeya, Tanzania Prisons watakua wenyeji wa vinara wa ligi hiyo
Young Africans katika uwanja wa Sokoine, Wana kimanumanu African Sports
watacheza dhidi ya Mwadui FC uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku
wakata miwa wa Kagera Sugar wakiwakaribisha Majimaji FC katika uwanja wa
Kamabarage mjini Shinyanga.
Alhamisi ligi hiyo itaendelea kwa kuchezwa mchezo mmoja tu, Wagosi wa
Kaya Coastal Union watawakaribisha Ndanda FC katika uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Michezo ya viporo ya Azam FC imepangiwa ratiba, mchezo dhidi ya
Tanzania Prisons utachezwa Februari 24 uwanja wa Sokoine jijini Mbeya,
huku mchezo dhidi ya Stand United ukichezwa Machi 16 katika uwanja wa
Azam Complex.