Timu ya Taifa (Taifa Stars) inacheza mechi ya kirafiki
na Botswana leo (Julai Mosi mwaka huu) kuanzia saa 9 alasiri kwa saa za huko.
Mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa jijini Gaborone
ni sehemu ya maandalizi ya Taifa Stars kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika
dhidi ya Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Julai 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager
inatarajiwa kurejea nchini Julai 6 mwaka huu kuendelea na programu nyingine kwa
ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji.
Wakati huo huo, kutakuwa na
utaratibu maalumu kwa waandishi wa habari za michezo kwa ajili ya kuripoti
mechi ya Stars dhidi ya Msumbiji. Hivyo, vyombo vya habari vinatakiwa kutuma
majina mawili ya waandishi watakaoripoti mechi hiyo. Mwisho wa kupokea majina
hayo ni Julai 8 mwaka huu.
WACHEZAJI WATANO WAOMBEWA ITC
Wachezaji
watano wameombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) ili waweze kucheza mpira
wa miguu nchini na nje ya Tanzania.
Abdulhalim
Humoud kutoka Simba, Crispine Odulla (Coastal Union) na Haji Ugando (Mbagala
Market FC) wameombewa ITC na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ili wakacheze
nchini humo katika klabu za Sofapaka, Bandari FC na Nakuru All Stars.
Vilevile TFF
imemuombea ITC mchezaji Ismaila Diarra kutoka nchini Mali ili aweze kujiunga na
timu ya Azam FC. TFF inafanyia kazi maombi hayo, na mara taratibu zote
zitakapokamilika itatoa ITC hizo kwa wachezaji wanaokwenda nje ya Tanzania.
SERENGETI BOYS
YAJINOA KUIKABILI AFRIKA KUSINI
Timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea
vizuri na mazoezi kujiandaa kwa mechi ya mashindano dhidi ya Afrika Kusini
(Amajimbos).
Mechi
hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itachezwa Ijumaa ya Julai 18 mwaka huu Uwanja
wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili
jioni.
Kocha
Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari ameshafanya mchujo wa awali wa
wachezaji wa timu hiyo kutoka 39 na kubaki na 31. Timu hiyo imepiga kambi
kwenye hosteli ya TFF iliyopo Uwanja wa Karume.
MBEYA CITY,
PRISONS KUJARIBU TIKETI ZA ELEKTRONIKI
Timu
za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) za Mbeya City na Tanzania Prisons zinacheza mechi
ya kirafiki Jumamosi (Julai 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine
jijini Mbeya.
Mechi
hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa jijini Mbeya katika mfumo wa matumizi ya
tiketi za elektroniki kwa washabiki wanaoingia uwanjani itaanza saa 10 kamili
jioni.
Kiingilio
ni sh. 3,000 kwa majukwaa yote ambapo tiketi zimeanza kuuzwa leo (Julai Mosi mwaka
huu).
Wakati
huo huo, keshokutwa (Julai 3 mwaka huu) kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya
tiketi za elektroniki yatakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini
Mbeya kuanzia saa 3 asubuhi.
Washiriki
wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa mechi katika uwanja huo, viongozi wa Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi
wake, makatibu wa Tanzania Prisons na Mbeya City, maofisa habari wa Mbeya City
na Tanzania Prisons, Ofisa Usalama wa MREFA na wasimamizi wa milangoni
(stewards).
BONIFACE WAMBURA MGOYO
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)