February 08, 2014

SERIKALI YATOA ONYO URAIS 2015.

Suala la baadhi ya viongozi nchini kuanza kampeni za kuwania urais mwaka 2015 kwa kumwaga fedha ili kujijengea mazingira ya ushindi, limechukua sura mpya baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuanza kuwabana.
Habari zilizolifikia gazeti hili na baadaye kuthibitishwa na Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, zinaeleza kuwa chombo hicho cha Serikali tayari kimewaita watu hao na kuwapa onyo baadhi yao wakiwamo mawaziri na wabunge walioanza kufanya kampeni.

Jaji Kaganda alisema kuwa waliwaita baadhi ya wanasiasa hao ambao wengi wana hadhi ya ubunge na kuwaonya kutokana na kubainika kwamba wanakiuka kanuni za maadili.
"Kwa upande wetu tumeshawaita baadhi, tulizungumza nao na kuwaonya kuhusu nyendo zao. Wapo waliotuelewa, naona wamekuwa kimya wakiendelea na shughuli zao nyingine za ujenzi wa taifa kwa nyadhifa walizonazo, ingawa pia wapo wengine tunasikia wanaendelea," alisema Jaji Kaganda.
Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepanga kuwachukulia hatua baadhi ya makada wake wanaodaiwa kuanza kufanya kampeni kabla ya wakati.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula wiki hii alikaririwa akiwa mjini Morogoro akisema kwamba tayari wamefungua mafaili ya watu wenye mitandao ya kampeni akisema wanaitambua mitandao hiyo hadi ngazi za mikoa na wataishughulikia.
Alisema kuwa muda wa kampeni za urais, udiwani, ubunge haujafika, hivyo wanaofanya kampeni sasa wanakiuka Katiba na Kanuni.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alipoulizwa kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaodaiwa kujipitisha kabla ya muda wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, alisema ofisi yake ipo tayari kuwashughulikia kwa mujibu wa utaratibu, ikiwamo kuwashtaki kwenye Sekretarieti ya Maadili, iwapo barua za malalamiko zitafikishwa kwake.
"Kwa jambo hili hatuwezi kuchukua hatua yoyote kama hakuna barua ya malalamiko iliyoletwa kwetu, hasa na vyama husika. Hivi sasa na sisi tumebaki tunaona na kusikia tu kwenye vyombo vya habari," alisema Jaji Mutungi.
Wiki iliyopita wabunge wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria walipokuwa kwenye ziara kwenye Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili, walihoji jinsi chombo hicho cha umma kilivyojipanga kuwashughulikia viongozi wanaodaiwa kumwaga fedha wakiwa katika maandalizi ya kugombea urais na ubunge.
Wabunge
Mjumbe wa Kamati hiyo, Nyambari Nyangwine ambaye pia ni Mbunge wa Tarime, alitaka kujua jinsi Sekretarieti hiyo, inavyoweza kuwashughulikia viongozi hao kwa kuwa vitendo hivyo vinakiuka maadili ya uongozi.
"Sekretarieti itawashughulikia vipi watu hawa ambao katika kuelekea Uchaguzi Mkuu, wameanza kampeni, wanamwaga fedha ili wapate uongozi?" Alihoji mbunge huyo.
Akijibu swali hilo, Katibu wa Utumishi wa Sekretarieti hiyo, Tixon Nzunda, alisema jukumu lao ni kushughulikia watu ambao tayari wana hadhi ya uongozi na kwamba zipo pia taasisi nyingine za Serikali zinazoweza kulifanyia kazi suala hilo.
"Ila pia kuna taasisi ambazo zinapaswa kuchukua hatua dhidi ya jambo hilo, kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa," alisema.
Aliongeza: "Sisi kwa upande wetu tumekuwa tukishirikiana na vyama hivyo, kwa kuwasisitizia viongozi wao kuhakikisha wanateua wagombea walio na sifa za maadili ili kulinda heshima na maana ya uongozi."
Kuhusu Sheria ya Kutenganisha Uongozi na Biashara, ambayo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliomba itazamwe upya, alisema mtu anayetaka kuwa kiongozi, anatakiwa kuepuka mambo yanayoweza kusababisha mgongano wa kimasilahi.
"Unapokuwa kiongozi lazima uyatambue mazingira yanayoweza kukusababishia mgongano wa kimasilahi, hivyo hatua hiyo ya kuzuia viongozi kuwa wafanyabiashara, siyo kwa sababu ya Azimio la Arusha, bali inalinda pia maadili ya kiongozi," alisema Nzunda na kuongeza;
"Hata hivyo, kuna mambo ambayo kiongozi mfanyabishara anatakiwa kuchagua moja kati ya matatu ambayo ni kuuza hisa zake katika kipindi cha siku 90 tangu kuchaguliwa, au aipeleke kwenye taasisi atakayoiamini na ajiondoe kusimamia au asikubali kuwa kiongozi."
Akitoa ufafanuzi juu ya hilo, Jaji Kaganda alisema, viongozi hawakatazwi kuwa matajiri, isipokuwa wanapaswa kujipatia mali kwa njia halali, kwa kuwa wakiwa na uwezo wa kipato, pia husaidia kutatua matatizo madogo ya watu wanaowaongoza.
"Naomba muelewe vyema, haikatazwi kiongozi kuwa tajiri, kwa sababu napo kiongozi akiwa maskini hataweza kuwasaidia wananchi kutatua matatizo yanayogharimu, hata kwa Sh10,000," alisema.
Chanzo:Mwananchi

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »