Chadema chawataka wafanyabiashara kutopandisha bei vyakula

July 16, 2013

Na Oscar Assenga, Tanga

MKURUGENZI wa haki za binadamu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje amewataka wafanyabiashara kuacha kupandisha bei vyakula kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuhamasisha chama hivi karibuni katika viwanja vya  Mwembe Mawazo, Bahweje amewataka wafanyabiashara hao kumkumbuka Mungu kwani mwezi huo ni waheri na baraka.

Amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakivitumia vipindi vya mwezi wa ramadhani kwa kupandisha bei vyakula na kujisahau kuwa ni mwezi wa Baraka na hivyo kuwataka kumkumbuka Mungu na  kuwapa wepesi wafungaji.

Amesema imekuwa kawaida kwa wafanyabiashara kuufanya mwezi wa Ramadhani kuwa ni kipindi cha kujitajirisha na kuwataka kuacha kufanya hivyo kwani kutasababisha kuwapa ugumu wafungaji.

Bahweje amewataka wafanyabiashara hao kuufanya mwezi huo kuwa ni wakutafuta Baraka na kupata malipo kutoka  kwa Mungu lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa waumini kufunga mwezi huo na kutouona mgumu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya, Khalid Rashid, aliwataka wakazi wa Chumbageni kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kuwaondoshea kero ambazo zinawakabili likiwemo wimbi la wizi wa madirishani usiku.
 
Amesema kero hiyo ambayo imeshindwa kupatiwa ufumbuzi na chama chenye Udiwani na hivyo kuadhimia kikifanikiwa kuchukua nafasi ya kuongoza kero hiyo itakuwa ya kwanza kuikomesha.

Amesema chama hicho kimeshindwa kuleta umoja na mshikamano na kuunda ulinzi shirikishi na badala yake matumaini ya kusogeza maendeleo yameshindikana na hivyo kuwataka wakazi hao kukiunga mkono chama hicho katika chaguzi zijazo.

Rashid amewataka wakazi hao kuacha kufanya makosa kwa kutokichagua Chadema kwani chama hicho kiko na sera za kumkomboa Mtanzania kutoka katika dimbwi la umasikini na kumuingiza katika maisha ya utajiri kwani nchi iko na rasilimali nyingi.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »