"RC Gallawa amuunga mkono DC Gambo sasa kuanzisha Gallawa Cup"

July 15, 2013
Na Oscar Assenga,Korogwe.

MKUU wa Mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa ameunga mkono Mashindano ya Gambo Cup ambapo amehaidi kuanzisha Mashindano ya Gallawa Cup ambayo yatachezwa mkoa mzima wa Tanga lengo likiwa ni kukuza na kuinua kiwango vya soka mkoani hapa

Kauli ya Mkuu huyo wa Mkoa aliitoa wakati wa fainali ya Mashindano ya Vijana ya Gambo Cup yaliyofanyika katika viwanja vya chuo cha ualimu wilayani hapa ambapo alisema mashindano hayo yalikuwa na msisimuko na dhahiri kufika lengo lililokusudiwa la kuinua viwango vya soka wilayani humo.

Gallawa alisema michezo hivi sasa ni ajira ambayo inaweza kuwainua vijana kutoka katika maisha ya chini hadi juu hivyo hawapa budi kuzingatia na kujifunza kwa moyo mmoja ili kuweza kupata mafanikio yatokanayo na soka ambayo ni makubwa sana.

Aidha mkuu huyo wa mkoa alimpongeza Mkuu wa wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo faida zake ni nyingi kwa vijana ikiwemo ajira,huleta undugu na kuwaepusha vijana kufanya vitendo viovu badala yake kwenda uwanjani kucheza au kuangalia mpira.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema Mashindano ya Gallawa Cup yataanza hivi karibuni na kila wilaya itapata fuksa ya kushiriki katika michuano hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kwani kila timu itahitaji kujipanga vema kwa ajili ya kuchukua ubingwa huo.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »