Na Oscar Assenga, Tanga.
IMEWEKWA JUNE 24 saa 12:11
UFINYU wa Bajeti ya
kutosha katika mradi wa uhamasishaji jamii kuhusu uchangiaji damu kwa hiari
katika wilaya za Korogwe, Mkinga na Tanga ni miongoni mwa changamoto
zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo likiwa linafanyika katika maeneo hayo hali
ambayo ilipelekea kutokufikia malengo yaliyokusudiwa.
Hayo yalisemwa na
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoani Tanga,(TPC)Hassani Hashimu hivi
karibuni wakati akisoma taarifa ya uhamasishaji huo kwa waandishi wa habari
kwenye majumuisho ya uchangiaji wa damu yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano
jijini Tanga .
Hashimu alisema katika
kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo ulifanikiwa kukusanya uniti 210 za
damu kati ya makadirio ya kukusanya uniti 450 ambapo kati yao wanaume
waliochangia ni 183 na wanawake walikuwa 27.
Aliongeza kuwa kutokana
na uhamasishaji huo uliofanywa na chama hicho katika kipindi chote cha
utekelezaji wa mradi huo kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya mkoa wa
Tanga wataalamu wa damu salama kutokana kanda ya kaskazini wameweza kukusanya
uniti 450 kati ya lengo walilojipangia la kukusanya uniti 1000.
Alisema kikwazo kingine
ni kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa uchangiaji wa damu ndani
ya jamii sambamba na kukosekana kwa msukumo kutoka kwenye mamlaka husika katika
kuvifanya vilabu vya wachangiaji damu kuwa endelevu.
Aidha aliiomba serikali
ya mkoa wa Tanga kupitia mganga mkuu wa mkoa kuweka utaratibu mzuri ambao
utawezesha wachangiaji damu wanaojitolea kwa hiari kutambulika na kupewa huduma
kwenye hospitali bila kikwazo pale inapohitajika.
“Tunaaamni kuwa huduma
bora hiyo itawafanya wachangiaji damu kuwa na ari ya kuendelea kujitolea kutokana
na kuwa na uhakika wa kupata huduma wakati wote wanapokuwa wakihitaji wao
pamoja na ndugu zao “Alisema Hashimu.
Alisema ombi hilo
linatokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wachangiaji damu kuwa wamekuwa
wakikosa huduma stahiki na ikibidi kununua damu hasa wanapohitaji huduma hiyo
kwenye hospitali za mkoani hapa.
Kampeni hiyo
ilizinduliwa mei 23 mwaka huu ambapo lengo kuu ilikuwa ni kukabiliana na
changamoto ya upungufu wa damu unaozikabili benki za damu katika hospitali za
mkoa wa Tanga hususani hospitali ya rufaa ya mkoa ambayo ni Bombo.
Mradi huo ulianzishwa na
Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Tanga( Tanga Press Club) kwa kufadhiliwa
na Kampuni ya simu za Mikononi ya Vodacom kwa kiasi cha shilingi milioni sita
6,000,000.
Mwisho.
EmoticonEmoticon