Kwamichi Fc yaitambia Mirado Fc

June 24, 2013

IMEWEKWA saa 01:44.

Na Mwandishi Wetu,Tanga.

TIMU ya soka Kwamichi Fc juzi ilifanikiwa kuchukua pointi tatu muhimu kwenye mechi yao na Mirada Fc baada ya kuibamiza mabao 3-0,ikiwa ni muendelezo wa michuano ya kombe la Sheshe Cup inayoendelea kutimua vumbi uwanja wa Chuda relini jijini Tanga.

Katika mchezo ambao ulikuwa na upinzani mkubwa licha ya Kwamichi Fc kuonekana kuutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na kupata bao lao la kwanza dakika ya 6 kupitia Omari Daiyo bao ambalo lilidumu mpaka timu zote zinakwenda mapumziko.

Mpaka timu zote zinakwenda mapumziko,Kwamichi walikuwa wakiongoza ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kutokana na timu zote kufanya mabadiliko.

Wakionekana kuukamia mchezo huo,Kwamichi waliweza kujipanga na kuweka safu imara ambayo iliweza kuwadhibiti wachezaji wa Mirada Fc hali iliyopelekea kuwachezesha nusu ya uwanja.

Kutokana na hali hiyo,Kwamichi waliweza kufanya shambulio la nguvu langoni mwa wapinzani wao na kuweza kufanikiwa kuandika bao la pili kwenye dakika ya 75 ambalo lilifungwa na Omari Bakata baada ya kutumia uzembe wa mlinda mlango wa timu ya Mirada na kuweka wavuni mpira huo.

Katika dakika ya 85 Yasini Baba Yero aliweza kuwainua kwenye vitini mashabiki wa timu ya Kwamichi mara baada ya kuifungia bao la tatu ambalo liliweza kuihitimisha karamu ya mabao.

Mratibu wa Ligi hiyo,Mbwana Sir Ride aliliambia gazeti hili lengo la kuanzishwa mashindano hayo ni kutaka kuibua vipaji vya wachezaji wachanga na kuinua kiwango cha soka.

MWisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »