Na Oscar Assenga, Tanga.
MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa
Tanga, Edson Makallo amesema endapo watanzania tutafanikiwa kudhibiti rushwa
kwenye michezo itasaidia kupata wachezaji wazuri wenye uwezo wa kuliletea sifa
taifa letu siku zijazo.
.Makallo alitoa rai hiyo jana wakati akifungua Mashindano ya
Vijana ya Takukuru Cup yaliyoanzishwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na chama
cha soka wilaya ya Tanga (TDFA) yenye lengo la kukuza na kuibua vipaji vya
wachezaji wachanga mkoani Tanga
Alisema rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo ya soka hapa nchini kutokana na kuwa mara nyingi huzifanya timu kushindwa kufanya maandalizi ya kutosha huku zikitegemea kupata ushindi wa kupewa badala ya kutumia jitihada zao binafsi wanapokuwa uwanjani.
Mkuu huyo alisema kuanzishwa kwa ligi hiyo ni kuhamasisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia michezo ambapo taasisi hao wakiwa kama wadau muhimu wanawajibu wa kukuza vipaji vya vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa katika taifa lolote lile duniani.
Aidha alisema wanatarajia kuanzisha ligi kubwa lengo kubwa
likiwa ni kutoa elimu juu ya mapambano dhidi ya rushwa kupitia michezo ili
wachezaji wafahamu kuwa rushwa ina athari gani katika jamii na inavyochangia
kurudisha nyuma maendeleo ya soka hapa nchini.
Makallo alisema mashindano hayo yalianza jana yakishirikisha
timu nne kutoka maeneo mbalimbali wilayani hapa na kuzitaja timu hizo kuwa ni Makorora
Sc,Veteren Sc,Bomboka Sc na Magomeni ambazo zitachukua ili kuweza kumpata
bingwa wa mashindano hayo.
Mshindi wa kwanza kwenye mashindano hayo atapata kombe na
jezi seti moja,mshindi wa pili atapata kitita cha sh.100,000,mshindi wa tatu
atapata sh.50,000 huku mshindi wa nne akipata sh.30,000.
“Suala la rushwa michezoni hudumaza maendeleo ya soka hapa nchini hivyo wanamichezo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupiga vita kwani ndio silaha yao ya kufikia malengo yao siku zijazo na Tanzania bila rushwa michezoni inawezekana “Alisema Makallo.
Mwisho.
EmoticonEmoticon