Tawi la Chama cha Mapinduzi Chuo kikuu Eckenforde kufunguliwa hivi karibuni

March 30, 2013

 


 


Na Oscar Assenga, Tanga
CHUO Kikuu cha Eckenforde-Tanga kinatarajia kufungua tawi la Chama cha Mapinduzi (CCM)  chuoni hapo katika kuitikia  azimio la Mkutano Mkuu wa CCM  wa kuanzishwa matawi  ya Chama kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu hapa nchini.
Akithibitisha habari hiyo, Katibu wa muda wa Jumuiya hiyo chuoni hapo, Rehema Maclean alisema Jumuia ya wananfunzi katika Chuo hicho wanatarajia kufungua tawi hilo baada ya kukidhi kigezo cha kufikia wanachama wanaozidi 50.
Maclean aliliambia blog hii jana kwamba sherehe za ufunguzi wa tawi hilo zinatarajiwa kufanyika mwezi Januari 5, mwaka huu lakini zimesongezwa mbele kutokana na sababu mbalimbali.
Akifafanua zaidi, Katibu huyo alisema kufunguliwa kwa tawi hilo Chuoni hapo kutaongeza idadi ya matawi kuwa mawili, ambayo ni pamoja na Chuo Kikuu cha SEKOMU kilichoko wilayani Lushoto.
Aidha, alisema kufunguliwa kwa tawi hilo ni kutekeleza azma ya kuunda mkoa wa Vyuo Vya Elimu  ya Juu kama ilivyoridhiwa na Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma mwaka huu.
 Hivi karibuni, akihutubia mkutano wa Jumuiya hiyo jijini hapa, Katibu wa Mkoa wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Christopher Ngu Ngubiagai alisema kufunguliwa kwa matawi ya Chama cha Mapinduzi katika Vyuo vya Elimu ya Juu ni hatua iliyochukuliwa kwa maksudi kwa lengo la kukisogeza Chama kuwa karibu zaidi na watu.
Alisema kuwa Chama kimedhamiria kuleta mageuzi makubwa yatakayoendana na dhamira ya kuwaingiza vijana katika safu ya uongozi wa nchi pamoja na mashirika na taasisi za umma.
Akasema vijana wana wajibu wa kulelewa kulingana na maadili ya Kitanzania na kuongeza kuwa uzalendo hauteremshwi kutoka mbinguni, bali hujengwa na moyo unaokataa rushwa.
 "Vijana wakijengewa uwezo wanaweza  kuongoza kwani wengi wao ni wazalendo wanaoipenda nchi yao kwa dhati”,alibainisha.  
Kwa kutambua hilo, alisema, tayari Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, J.K. Kikwete  ameanza kuwaingiza vijana katika nafasii mbalimbali za uongozi wakiwemo Wakuu wa Wilaya ambao wanaongoza kwa wingi katika safu hiyo.
Katibu huyo wa Mkoa wa Vyuo Vya Elimu ya Juu alifafanua kuwa CCM mlango wa kujenga mahusiano ya karibu baina ya wanafunzi hao wa Vyuo Vya Elimu ya Juu na CCM.
Alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa Mkoa wa Vyuo vya Elimu ya Juu ni kueneza itikadi ya CCM pamoja na kujenga uzalendo na maadili ya kitaifa.
Hata hivyo Ngubiagai alitahadharisha kwamba shughuli zote za kisiasa zitafanyika nje na maeneo ya Vyuo na kwamba wanachama ni vanavyuo tu.
Katibu wa Muda wa Tawi hilo,Rehema Maclean alisema wanachama hao tayari wamejiandaa kikamilifu tayari kwa ufunguzi wa tawi lao ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
 (Mwisho).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »