NUNDU awapa muda wa miezi mitatu wananchi.

March 30, 2013

Na Oscar Assenga, Tanga.
MBUNGE wa Jimbo la Tanga,Omari Nundu amewapa muda wa miezi mitatu wananchi waliochukua fedha katika mfuko wa  Zindaba Fund wawe wamekwisha kuzirejesha la sivyo watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wake na wananchi wa kata za Marungu,Kirare,Tongoni na Tangasisi ziliyopo jijini Tanga alisema wananchi hao wamechukua fedha hizo na kushindwa kuzirejesha licha ya kuandikiwa barua za mara kwa mara kufanya hivyo bila kuwepo kwa mafanikio yoyote yale.

Hatua ya mbunge huyo ameichukua kutokana na wananchi hao mbalimbali jijini Tanga kuchukua fedha katika mfuko huo kiasi cha sh.milioni 78 huku baadhi yao wakirudisha nusu nusu na wengine wapatao 33 wakishindwa kuzirudisha fedha hizo ili ziweze kuwasaidia na wananchi wengine shughuli zao mbalimbali.

Alisema hata akichukiwa na mtu yoyote hatajali badala yake ataendelea kufanya kazi ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia kwa wakati pamoja na kufanyia kazi changamoto zinazowakabili.

Akizungumzia tatizo la usalama nchini,Nundu alisema haiwezekani makanisa yakachomwa moto na serikali kuendelea kuyafumbia macho na kuitaka serikali kuangalia uwezekano wa kuywazibiti wahalifu wa aina hiyo ili kudumisha hali ya usalama na amani hapa nchini.

Aidha pia alitumia fuksa aliyoipata kuwaasa viongozi wa vyama vya upinzani wanapokuwa kwenye mikutano yao waongelee sera na sio mambo mengine yasiyo na tija kwa wananchi wao.

    “Tunapotaka kuwaletea maendeleo wananchi wetu tusiangalie itikadi za vyama vyetu bali tuangalie namna ya kufanya ili wananchi tunaowaongoza waweze kupata unafuua wa maisha kwa  kuangalia jinsi gani tunaweza kutatua kero zao zinazowakabili “alisema Nundu.

Katika mkutano huo,mwananchi wa kata hiyo,Abdallah Mnyamisi alimueleza mbunge huyo kuwa wanamatatizo kwenye ofisi yake hakuna watendaji wazuri na kumuomba mbunge huyo kuwa fedha zake za mfuko wa jimbo azipeleke katika kutatua kero mbalimbali za wananchi vijijini.

Akijibu swali hilo,Nundu alihaidi kuzifanyia kazi changamoto zote zinazowakabili wananchi katika maeneo yao kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi ya vijiji na kata ili kuweza kuyapatia ufumbuzi kwa haraka iwezekanavyo.

Awali akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga,Kassimu Mbuguni alisema pamoja na mbunge huyo kufanya mkutano huo lakini pia walienda kusikiliza ilani ya chama hicho na kuhaidi kuyafanyia kazi maneno yaliozungumzwa na wananchi katika mkutano huyo ili yaweza kufikia malengo yao.

Mwisho

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »