WANANCHI wamkaanga diwani mbele ya DC

March 30, 2013

Na Oscar Assenga, Lushoto.

WANANCHI wa Kijiji cha Ungo Kata ya Mlola wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamelazimika kumueleza Mkuu wa wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga kuwa diwani wa Kata hiyo, Shekallage Rashid amekuwa akishindwa kusimamia miradi ya maendeleo na hivyo kumuomba kumuajibisha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya msingi iliopo kwenye kijiji hicho ikiwa ni ziara yake ya siku nne ya mkuu huyo wa wilaya ya kukagua miradi ya maendelo na kusikiliza kero za wananchi zinazowakabili.
Wananchi hao walisema kuwa waliazimia kujenga zahanati na waliamua kupanga kuwa wananchi wanaoishi katika kijiji hicho wawajibike katika kutengeneza matofauti ambayo yatajengea zahanati hiyo.

Akizungumza mmoja wa wananchi wa kijiji hicho,Rashid Mtangi alimueleza mkuu huyo wa wilaya kuwa baada ya kukubaliana hivyo walianza kazi hiyo mara moja na kufanikiwa kufetua matofali na kuyaweka karibu na eneo la shule kwa ajili ya ujenzi huo na kuchukua muda wa kipindi cha miaka miwili lakini ukashindwa kufanyika na matofauti hayo kuharibika.

Mtangi alisema kutokana na kitendo hicho wananchi wa eneo hilo huenda wakashindwa kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao kutokana na viongozi wazembe ambao wanashindwa kusimamia majukumu yao na kusababisha nguvu za wananchi kupotea.
  “Diwani wetu haitishi hata mikutano ya wananchi kitendo ambacho kinawafanya wananchi kushindwa kuona umuhimu wao katika nafasi wanazoziongoza kwani hawaelewi anafanya kazi gani kwao“Alisema Mtangi.

Aidha aliongeza kuwa kijiji hicho kimekuwa hakina mtendaji kwa muda mrefu hali ambayo inapelekea wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kushindwa kuelezwa mapato na matumizi yao kwa muda mrefu na hivyo kuchangia kurudisha nyuma kasi ya maendeleo.

Akijibu tuhumu hizo,Diwani Rashid alimueleza Mkuu wa wilaya kuwa  hakuna mahali popote alipokwamisha ujenzi za zahanati hiyo bali aliambiwa na mbunge wa jimbo hilo,Henry Shekifu na mganga mkuu wa wilaya hiyo aliyehamia kilombero mkoani Morogoro kuwa kuwa umbali wa kituo cha Afya cha Mlola na eneo ambalo kulitakwa kujengwa zahanati hiyo ni karibu.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga alisema hatamuangalia tu kwa cheo chake wala thamani aliyonayo katika jamii kutokana na kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi atahakikisha wachukulia hatua zinazostahili.

    “Watu wanataka serikali ichukiwe kuwa haikufanya kitu kutokana na watendaji wazembe hatutokubali hali hii iendelee lazima wale wote ambao wanakwamisha miradi ya maendeleo ya wananchi wachukuliwe hatua stahiki “Alisema DC Mwanga.

Mwanga aliwaomba wananchi wampe muda aende akaangalie kuwa mradi huo wa zahanati hiyo na kuwataka viongozi mbalimbali katika kata hiyo kuheshimu maamuzi ya serikali hasa za vijiji.

Aidha alisema suala la wananchi wao kutokuwa na mtendaji kwa muda mrefu alihaidi kulishughulikia na kubwa baraza la madiwani walikumbushie ili liweze upata ufumbuzi haraka iwezekanayo.

Akizungumzia suala la wanafunzi ambao hawajaripoti mashuleni tokea shule hizo zilipofunguliwa aliwaagiza watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yote wilayani humo kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti haraka iwezekanavyo na wampelekee taarifa zao ofisini wake.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »