MKUU wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi katika fainali ya Mashindano ya Kombe la Vijana ya Gambo Cup
itakayofanyika katika uwanja wa Chuo cha Ualimu wilayani hapa.
Akizungumza jana,Mratibu wa Mashindano hayo,Zaina Hassani alisema
maandalizi ya hatua hiyo yamekamilika ambapo leo (jana)kutachezwa mechi ya
kumtafuta mshindi wa tatu kati ya Bungu Kibaoni na Kosovo Fc.
Hassani alizitaja timu ambazo zitacheza hatua ya fainali ya
mashindano hayo kuwa ni Korogwe United ambao ni mabingwa wa soka wilaya ya
Korogwe watakuwa na kibarua kizito dhidi ya Mtonga Fc mchezo unaotazamiwa kuwa
na upinzani mkubwa.
Katibu huyo alisema mshindi wa kwanza katika mashindano hayo
anatarajiwa kuondoka na Ng’ombe ,Kombe,Jei seti 1 na mipira 2,mshindi wa pili
anatarajiwa kuondoka na Mbuzi wawili,jezi seti moja na mpira mmoja huku mshindi
wa tatu akitarajiwa kuondoka na Mbuzi 1,Jezi seti 1 na mpira 1.
Aliongeza kuwa kuanzia mshindi wanne hadi wa nane wanatarajiwa
kupata Jezi seti 1 na mpira moja moja kila timu ikiwa ni kuzipa chachu ya
kufanya maandalizi ya msimu mpya ambao utaanza mara baada ya kumalizika msimu
huu.
Mashindano ya Gambo Cup yalianzishwa na Mkuu wa wilaya ya
Korogwe, Mrisho Gambo na kufadhiliwa na benki ya NMB lenye lengo la kukuza na
kuinua vipaji vya wachezaji wachanga wilayani humo ambapo yalishirikisha timu
85 kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo.
Mwisho.