Na Oscar Assenga, Tanga.
UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga umetimua rasmi
wajumbe wa kamati ya utendaji wa timu hiyo ambao walichaguliwa katika uchaguzi
mkuu mwaka uliopita kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Akitangaza uamuzi wa kuwafukuza katika mkutano mkuu wa
wanachama mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Hemed Aurora alisema
hatua hiyo inatokana na wajumbe hao kuwa mzigo katika nafasi zao ikiwemo
kushindwa kuhudhuria vikao vya kamati tendaji tokea walipochaguliwa.
Kauli ya Aurora inafuatia na swali aliliulizwa na Mwanachama
wa Klabu hiyo, Miraji Wandi aliyetaka kujua uongozi wa timu hiyo umewachukuliwa
hatua gani viongozi ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao hali ambayo
inapelekea kuwa mzigo kwa klabu hiyo?
Aurora alisema tayari wameandaa utaratibu wa kuandika barua
kwa ajili ya kuwatimua rasmi katika nafasi zao hizo pamoja na kutangaza nafasi
za hizo katika uchaguzi mdogo ambao utafanyika hivi karibuni kuziba mapengo
hayo.
Aidha mwenyekiti huyo aliwataka viongozi waliopo katika klabu
hiyo na wanachama kila mmoja kutimiza majukumu yake ili kuweza kusukuma
gurudumu la maendeleo ya timu hiyo ambayo imedhamiria msimu ujao kuchukua
ubingwa.
Mwenyekiti huyo aliwataja wajumbe wa kamati ya utendaji ambao
wamewatimuliwa ni Julius Benjamini na Nashoni Kweli ambao tokea wachaguliwe
katika nafasi zao wamekuwa wakishindwa kutekeleza majukumu yao.
Mwisho.