VICTORIA GWARA: SHUJAA WA HEDHI SALAMA ANAYEIPIGANIA JAMII YAKE

April 18, 2024

Mohammed Hammie Rajab.

Hedhi salama si jambo linalozungumzwa kwa kiasi kikubwa hususani katika jamii nyingi za kitanzania, hii ni kutokana na imani za kidini, mila pamoja na tamaduni.

Licha ya kuwepo kwa kampeni na harakati nyingi zenye lengo la kuelimisha wanawake na wasichana juu ya hedhi salama hapa nchini, lakini bado kumekuwa na changamoto ya ufikaji wa elimu hiyo hasa maeneo ya vijijini.

Jitihada zinazofanywa na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya hedhi salama ni kielelezo tosha cha kuisaidia serikali pale ambapo kumekuwa na ufinyu wa ufikiwaji wa maeneo hayo kwa ajili ya kutoa elimu.

Victoria Gwera kutokea kijiji cha Mgudeni wilayani Kilombero mkoani Morogoro ni miongoni mwa wanawake waliowahi kufikiwa na elimu ya hedhi salama, mafunzo aliyoyapata kutokea shirika la CEMDO lililopo Ifakara mkoani humo.


Bi Victoria Gwera akiwa kwenye tabasamu. Moja ya picha iliyopigwa akiwa kijijini kwake Mgudeni anapoishi.

Mbali na elimu hiyo, Victoria na washiriki wengine walipatiwa pia mafunzo ya kutengeneza tauli za kike (pedi) kwa kutumia vitenge pamoja na sabuni ambazo kwa mujibu wa lengo la mafunzo hayo zingewasaidia kwenye usafi wakati wote wa hedhi.

Baada ya mafunzo hayo Victoria aliamua kufanya kitu cha kipekee kwa jamii yake ambacho mpaka sasa kinaendelea kuacha alama.

“Niliporudi kijijini baada ya kupata mafunzo, niliamua kuanza kutengeza pedi na sabuni kwa ajili ya matumuzi yangu na jamii kwa kuuza kwa bei rahisi” anasema Victoria wakati wa mazungumzo maalumu na mwandishi wa makala hii.

Anasema ilimchukua muda wa miezi miwili tu kufanyia kazi mafunzo ya utengenezaji wa pedi hizo na sabuni, kuzijaribu, kuzitumia yeye mwenyewe kwanza kabla ya kupata wazo la kuanza kusaidia wanawake na wasichana wanaokumbana na changamaoto ya gharama za pedi wakati wa hedhi.

(Bi Victoria Gwera akiwa kwenye shughili zake za utengenezaji wa tauli za kike nyumbani kwake Mgudeni.

Victoria angeweza kuyapiga teke maarifa aliyoyapata na kusingekuwa na mtu wa kumuuliza, huenda pia ilikuwa hivyo kwa washiriki wingine, lakini yeye kuna kilichomsukuma mpaka akaamua kufanya kitu cha pekee.

“Wakati nipo msichana mdogo niliwahi kupatwa na changamoto ya kukosa pedi, gharama zilikuwa kubwa kulinganisha na hali ya familia yetu, hivyo kila nikikumbuka hali hiyo huwa naumia. Sitaki wasichana na wanawake wengine hapa kijijini wapitie yale niliyowahi kupitia mimi na ndio maana nikaamua kutengeza hizi pedi na sabuni na kuuza kwa bei rahisi” anasema Victoria.

Inaelezwa kuwa moja kati ya nyenzo za msingi ili kufanikisha hedhi salama ni elimu sahihi, upatikanaji wa taulo za kike (pedi), sabuni pamoja na maji safi na salama, vitu ambavyo Victoria mbali na kuvikamilisha, pia anawasaida wanawake wenzake kukamilisha.

“Mimi nimepata mafunzo ya hedhi salama, kwa hiyo ninapokwenda kuuza hizi pedi huko maeneo ya kijijini huwa natoa na elimu pia. Inawasaidia sana wasichana wanaoingia kwenye hedhi kwa mara ya kwanza” anasisitiza Victoria.

Kwa kutumia baiskeli, Victoria husafiri zaidi ya kilomita tano kwa siku ili kuwafikia wateja wake, wengi kutokea kijiji alichopo na vijiji jirani ambavyo anaamini bado elimu ya hedhi salama haijafika kwa kiwango kikubwa. Pedi tatu akiuza kwa kiasi cha shilingi za kitanzania elfu moja.


Bi Victoria Gwera akielekea kwenye biashara yake ya kuuza tauli za kike na sabuni

Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Tanzania wanawake Milioni 13,750,122 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 hupata hedhi kila Mwaka. Ikielezwa kuwa idadi hiyo ni kubwa na hivyo jamii ina kila sababu ya kuhakikisha kuwa kundi hilo linapata huduma bora wakati wa hedhi ikiwemo kuhakikisha uwepo wa maji, sabuni na taulo za kike ili kufanya hedhi iwe salama kwao.

Hivi karibuni Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwenye maadhimisho ya wiki ya hedhi salama duniani alitoa wito kwa jamii kuwa na uelewa kuwa hedhi sio balaa, ugonjwa wala sio laana bali ni mabadiliko ya hali ya kawaida yanayomtokea mwanamke au msichana mara baada ya kubalehe kama ishara kwenye mfumo wa maumbile yake ya uzazi.

Victoria Gwera anawakilisha wanawake wengine wengi nchini Tanzania ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kuikomboa jamii yao na changamoto ya hedhi salama kwa kuonekana ama kutoonekana. Hivyo ni vyema serikali na wadau wengine kuenzi na kuendeleza jitihada hizi ili kuwanusuru wanawake na wasichana.

Mwisho

Mohammed Hammie Rajab
A Human Rights to Water Journalist
(Equal Water Voice To All)
Phone: +255719000010

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »