Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera amewataka viongozi wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, kufanya mikutano vitongojini ili kubaini, kero, migogoro na changamoto za jamii ili wazitatue.
Dk Serera akizungumza na wakazi wa kitongoji cha Getini mji mdogo wa Mirerani, amesema viongozi wa mamlaka ya mji mdogo wanapaswa kushiriki kwenye mikutano ya vitongoji ili kusikiliza kero za watu.
"Hatuwezi kutatua mgogoro, kero na changamoto za jamii kwa kukaa ofisini hivyo viongozi wa mamlaka fanyeni mikutano ili mtatue matatizo yao," amesema Dk Serera.
Amesema viongozi wasipofika chini na kufahamu matatizo ya watu hawataweza kuyatatua hivyo wabadilike kwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Isack Mgaya amesema wataweka utaratibu wa kufanya mikutano hiyo ili kutekeleza agizo hilo.
"Awali mara moja moja tulikuwa na utaratibu wa kufika kwenye mikutano ya kitongoji inayoandaliwa katika vitongoji kila baada ya miezi mitatu," amesema Mgaya.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi ameishukuru serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa kituo cha afya kitakachosogeza huduma za afya kwa ukaribu.
"Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea kituo cha afya ili kuepusha wanawake wajawazito na watoto kufuata huduma za afya umbali mrefu," amesema Mnyawi.
Mkazi wa kitongoji cha Msikitini, Adam Komba ameiomba serikali kutafuta namna ya kuyadhibiti maji ya bwawa la kidawashi kwani yanasababisha mafuriko.
"Maji ya mto Nduruma yamedhibitiwa na bonde la mto Pangani kwa kuchimba mtaro mkubwa unaopitisha mkondo wa maji yake hadi mto Kikuletwa ila hayo mengine ndiyo yanasababisha mafuriko," amesema Komba
EmoticonEmoticon