NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa juhudi zake za kuimarisha diplomasia inayoongeza fursa za kiuchumi zinazoleta tija na mafanikio kwa pande zote za Muungano.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,wakati akitoa tathimini na uchambuzi wa fursa na mafanikio ya Tanzania Kimataifa kupitia mahojiano yaliyofanyika katika Kituo cha Radio ya Bahari FM,kilichopo Migombani Zanzibar.
Mbeto,alifafanua kuwa Rais Dkt.Samia,ameendelea kuipaisha Tanzania kiuchumi ili ifike katika kilele cha maendeleo endelevu sambamba na kupata hadhi ya nchi iliyoendelea kiuchumi Barani Afrika.
Alisema Chama Cha Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar kinapongeza kwa dhati juhudi,maarifa,ubunifu na uchapakazi wa Rais wa Dkt.Samia na kwamba utendaji huo uliotuka ndio kibali cha Wananchi kumpa ridhaa ya kushinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika maelezo yake Katibu huyo wa NEC,aliwasihi Wananchi bila kujali tofauti za kisiasa,kidini na kikabila kumuunga mkono kwa kila hatua anayopiga katika kutafuta fursa mbalimbali kupitia ziara,makongamano na mikutano ya kimataifa.
Katibu huyo mwenezi alisema kupitia ziara zake amekuwa akitangaza fursa za Utalii kupitia dhana za Royal Tour na Uchumi wa Buluu zinazofafanua kwa kina rasilimali zilizopo nchini zikiwemo mbuga za wanyama,Bahari,mito,maziwa,vivutio vya mambo ya kale ili raia wa kigeni waje kwa wingi nchini kwa ajili ya Uwekezaji na utalii.
" Najua wapo baadhi ya watu wachache wanakosoa na kubeza juhudi hizi za Rais Dkt.Samia,wakidai anafanya ziara nyingi nchi za nje lakini tukumbuke kuwa ziara hizo sio za kifamilia bali anaenda kutafuta fursa za kiuchumi na kuimarisha mahusiano mema ya kidiplomasia yakiambatana kuingia na mikataba mikubwa yenye tija kwa nchi.
Alisema bajeti Kuu ya Tanzania kwa mara ya kwanza imefikia kiasi cha zaidi ya Trioni 41 ambapo asilimia 35 imeelekezwa katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha Wananchi.
Mbeto,akizungumzia ziara za Rais Dkt.Samia,Makao Makuu ya dhehebu la dini ya Kikiristo Vatican,amesema imejenga mahusiano makubwa na kudhihirisha kuwa kiongozi huyo hana ubaguzi anajali imani za dini za wananchi wote.
Alieleza kuwa pamoja na hayo ziara hiyo ya kukutana na Papa Francisko wamekubaliana kuongeza miundombinu ya kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa skuli,vyuo vikuu,hoteli kubwa za kitalii na viwanda vitakavyowanufaisha wananchi wote.
Pia ziara nyingine ya nchini Norway imeendelea kufungua fursa mpya za kiuchumi zikiwemo Uwekezaji katika Sekta za uvuvi pamoja na kuingia mikataba ya kushirikiana katika teknolojia ya masuala ya Gesi na Mafuta nchini.
Mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa makubaliano na Wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ibara ya 132 (a)-(e) imeelekeza katika kipindi Cha miaka mitano ijayo,CCM itahakikisha kuwa mahusiano ya nchi kikanda na kimataifa yanaendelea kuimarishwa lengo Kuu ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha Amani,uhuru na maslahi ya Taifa katika nyanja za kimataifa.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis.
EmoticonEmoticon