WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA UBUNIFU UANDISHI MATOKEO YA SENSA

September 18, 2023

 

Na Mwandishi Wetu – Njombe

Waandishi wa Habari nchini wameaswa kuzingatia weledi katika kuandika habari za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa Waandishi wa Habari wa mikoa ya Njombe na Ruvuma leo Septemba 18, 2023 mjini Njombe, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka amesema kuwa Waandishi wa Habari wana nafasi kubwa ya kuwawezesha wananchi kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 kujiletea maendeleo.

“Zingatieni mafunzo haya ili yawasaidie kujenga uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina kwenye takwimu zinazotolewa baada ya Sensa ya mwaka 2022 ili zisaidie katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kuwa watafanya maamuzi sahihi na yenye tija kwa kutumia matokeo yanayotolewa na jukumu lenu ni kuwafanya wananchi kuyaelewa,” alisisitiza Mhe. Mtaka.

Akifafanua amesema kuwa, waandishi wana nafasi kubwa ya kutumia ubunifu na mafunzo ya kuwajengea uwezo, kuwawezesha Wananchi kuongeza kasi ya kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla ikiwa watatimiza wajibu wao wa kuwahabarisha wananchi taarifa sahihi na kwa wakati.

Akiwasisitiza waandishi hao kuhusu umuhimu wa kubadilika Mhe. Mtaka amesema ulimwengu umebadilika na mahitaji yamebadilika kutokana na kukua kwa Sayansi na Teknolojia, hivyo na uandishi wa sasa unahitaji kufanya uchambuzi wa takwimu kwa usahihi ili kusaidia watakaotumia takwimu hizo kuleta matokeo chanya kwenye jamii.

Sanjari na hilo, Mhe. Mtaka amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia yote watakayojifunza ili yawasaidie kuwa chachu ya kuleta mabadiliko.

Akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mtakwimu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Israel Mwakapalala amesema kuwa mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na, uchambuzi wa takwimu za sensa kwa ajili ya habari, usambazaji wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Kidigitali, wajibu wa Vyombo vya Habari katika kusambaza Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, majukumu ya NBS, Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na mwongozo wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mafunzo hayo ya siku 2 yameshirikisha waandishi wa habari takribani 70 kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »