Na. Saidina Msangi, WF, Busan, Korea Kusini.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inatarajia kusaidia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kipande cha Tabora – Kigoma (lot 6) na Uvinza – Malagarasi (lot 7) kwa takribani dola za Marekani bilioni 3.05 na kufadhili maandalizi ya mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Mangapwani Zanzibar kwa takribani dola za Marekani milioni 60.
Hayo yameelezwa na Rais AfDB, Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango – Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya, pembezoni mwa vikao vya mkutano wa saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC), Mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini.
“Benki ya Mandeleo ya Afrika inafanyia kazi upatikanaji wa kiasi cha dola za Marekani bilioni 3.05 kwa wakati ili kuwezesha kutekelezwa kwa mradi wa SGR kwa manufaa ya Tanzania pamoja na nchi za jirani”, alieleza Dkt. Adesina.
Akizungumzia kuhusu ushirikishwaji wa Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi, Dkt. Adesina alisema kuwa kuna umuhimu wa kuhusisha sekta hiyo katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini Tanzania ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukuza uchumi.
Dkt. Adesina alisisitiza kuwa ni vyema kuendeleza sekta binafsi kwa kuwa ni muhimu katika kukuza uchumi kwa kasi na pia akaishauri Serikali kutumia fursa ya dirisha la AfDB (non- Sovereign Window) kwa ajili yakuimarisha na kuwezesha sekta binafsi nchini.
Aidha, alieleza kuwa Benki ya AfDB ipo tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kupiga hatua kimaendeleo hasa katika miradi ya Kilimo, huku akiutaja mradi wa Kilimo wa Building Better Tomorrow (BBT) kuwa utatoa ajira kwa vijana wengi na kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango – Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akiongoza ujumbe wa Tanzania kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuongezea Tanzania mgao wa fedha kupitia dirisha la mikopo nafuu (ADB) kwa mwaka 2023 kutoka UA 160 milioni sawa na dola za Marekani milioni 216 hadi UA 560 milioni sawa na dola za Marekani milioni 756.
Dkt. Mkuya alieleza kuwa kutokana na umuhimu wa miradi ambayo AfDB imeonesha nia ya kuifadhili hususani mradi wa ujenzi wa bandari ya Mangapwani Zanzibar, ameiomba Benki hiyo ione namna ya kuweza kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kabla ya mwaka 2025.
‘’Tayari tumefanya upembuzi yakinifu katika mradi wa bandariya Mwangapwani hivyo upatikanaji wa fedha utawezesha mradi huo kuanza mara moja”, alieleza Dkt. Mkuya.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina, akipokea zawadi kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango – Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, baada ya mazungumzo yao walipokutana pembezoni mwa vikao vya mkutano wa saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC), Mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina, akimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango – Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akizungumza walipokutana pembezoni mwa vikao vya mkutano wa saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC), Mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango – Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, na Balozi wa Tanzania Jamhuri ya Korea Kusini Mhe. Togolani Mavura.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina, akiagana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango – Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo yao walipokutana pembezoni mwa vikao vya mkutano wa saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC), Mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina, akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango – Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, na ujumbe kutoka Tanzania na AfDB, mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo yao walipokutana pembezoni mwa vikao vya mkutano wa saba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na Nchi za Afrika (KOAFEC), Mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Busan, Korea ya Kusini)
EmoticonEmoticon