Na Mashaka Mhando, Tanga
SERIKALI kwa kushirikiana na Project Inspire ipo kwenye mchakato wa kujenga kituo kikubwa cha Sayansi na teknolojia Mkoani Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teklonojia Profesa Adolf Mkenda alisema jana kwamba kituo hicho kitatumiwa na viongozi wengine wa serikali kama mfano utakaosaidia vituo vya aina hiyo kujengwa maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wanafunzi kusoma na kupenda masomo ya sayansi.
Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea kituo cha sayansi cha Stem Park kilichopo jijini Tanga, na kwamba mpango huo utasaidia kumaliza tatizo la wanafunzi kutopenda masomo ya sayansi wanapokuwa shuleni.
Waziri Mkenda alisema kituo hicho kitajengwa mjini Dodoma kitakuwa kama kituo cha mfano ambacho wabunge na viongozi wengine wa serikali watakitembelea ili kuona umuhimu wa kuwa na vituo vya aina hiyo kwenye maeneo yao.
"Dodoma ni katikati ya nchi yetu halafu pale wabunge, mawaziri wenzangu na watu mbalimbali wakuu wa mikoa nitapenda watembelee waone nini kinaweza kufanyika vituo hivi vinapaswa kujengwa kila mkoa najua haitafikia wanafunzi wote vitu vyote hivi ni matumda ambayo yanapatikana kirahisi, "alisema Waziri Mkenda.
"Kwahiyo mimi mwenyewe nitasapoti kwanza tutafute eneo jijini Dodoma litupe eneo na majengo waje pale na tusiwatoze hata thumni kwasababu wenyewe hawawatozi wanafunzi wanaokuja kufanya mafunzo hapa hawalipishwi chochote,"alisisitiza Prof Mkenda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Project inspire Lwidiko Edward alisema kituo hicho kinawatengeneza wanafunzi kwenye masomo ya sayansi kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kujifunza kwa miradi na kuandaa mazingira yanayotoa hamasa ya kusoma.
Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Amos Nungu alisema kituo hicho kitasaidia kujenga mapenzi ya watoto kupenda masomo ya sayansi tokea wakiwa katika umri mdogo.
Mpango wa ujenzi wa vituo hivyo unakuja wakati kukiwa na ari ndogo ya wanafunzi wanaopenda masomo ya sayansi ambao wengi wamekuwa wakikimbilia masomo ya sanaa kutokana na mazingira duni ya kujifunza masomo hayo.
Mwisho.
EmoticonEmoticon