MKUU wa Idara ya Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Sinde Mtobu
Na Oscar Assenga,TANGA.
MKUU wa Idara ya Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Sinde Mtobu amewaomba viongozi mbalimbali wa kijamii wakiwemo Wakuu wa Mikoa,Wabunge na Madiwani kuhamasishaji wananchi kuchangia damu na kuifanya kama sehemu ya agenda yao wanapokuwa katika matukio mbalimbali ya kijamii.
Pia amewasihi viongozi wa dini kutumia maeneo yao ya ibada kuhamasisha waumini kuchangia damu ikiwemo kuandaa matukio mbalimbali ya uchangiaji damu kwa sababu wananchi wanawaamini sana viongozi wao na hivyo itakuwa ni njia rahisi watoa huduma kupata damu ya kutosha kuwahudumia wahitaji.
Hatua hiyo inaweza kusaidia kwa asilimia kubwa wananchi kuwa na mwamko wa kuchangia damu na hivyo kuwezesha benki za damu kuwa na utoshelevu ambao utasaidia wahitaji wanapojitokeza.
Mtobu aliyasema hayo wakati akizungumza kuhusu umuhimu wa wananchi kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watanzania wengine ambapo alisema viongozi hao iwapo wakiitumia vizuri agenda hiyo ya kuandaa na kuwahamasisha katika mikutano na mikusanyiko mbalimbali wanayoifanya kwenye maeneo yao itasaidia jamii kuwa na mwamko wa kuchangia damu
Alisema wanawaomba viongozi wa dini wawasaidie maana wao wana watu wa kutosha wanaowaamini wakisimama kwenye maeneo yao na kuhamasisha wananchi kuchangia na wakati kuratibu matukio ya yatakayohusisha uchanguaji wa damu.
“Katika hili niwaombe viongozi wetu wa Kijamii, Serikali za Mitaa, Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa, Wabunge, Wakuu wa Wilaya na Mikoa kufanya matukio ya uchangiaji damu kuwa agenda yao ya jamii wanapokuwa na matukio ya watu kwa kuhamasisha jamii katika kuchangia damu.” Pia aliongeza kuwa, jamii ina hofu juu ya ushiriki wa kuchangia damu, hivyo viongozi wetu wa kijamii wakiwa katika msitari wa mbele wa kuchangia kwa vitendo na kuhamasisha, hakika mwitikio na hamasa kubwa itakuwepo toka kwa wananchi, alisema ndugu Mtobu.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Idara alivitaka pia vyombo vya habari kuhamaisha na kuwaita wataalamu ambao watasaidia kutoa elimu ya umuhimu wa kuchangia damu kwa kuhamasisha jamii kuchangia damu kwa hiari mara nyingi iwezakanavyo.
“Ndugu zangu tendo la kuchangia damu ni la imani na thawabu mbinguni maana unakuwa umeokoa uhai wa mtu ni suala la kiimani hivyo niwaase wananchi wenzangu tuwe na mwamko wa kuchangia damu kuokoa maisha ya wenzetu wahitaji walau mara tatu kwa wanawake na mara nne kwa wanaume kwa mwaka” Alisema.
Aidha pia aliitaka Jamii kuwa na mwamko wa kuchangia damu ili kuwa sehemu ya kuokoa uhai wa wengine ambao ni wahitaji
Mtobu alisema katika Hospitali hiyo, wanatoa huduma za kitabibu zinazohitaji matibabu tofauti tofauti kwa mfano huduma ya damu ni moja ya tiba muhimu kwa wagonjwa wenye uhitaji wa damu kama ilivyo tiba ya dawa.
Alisema hospitali ya Rufaa kwa mwezi inatumia damu wastani wa chupa 500 mpaka 600 za damu lakini uwezo wa kuchangisha damu kutoka kwa wananchi kwa hiari mara nyingi chupa 200 mpaka 300. Mtobu alisema upungufu huo unahitaji wananchi kujitokeza kwa wingi waweze kupata damu ya kutosha. Aliiasa jamii kuona umuhimu wa kuchangia damu. mara kwa mara kwa kuwa matumizi ya tiba damu yapo wakati wote katika kuwahudumia wagonjwa.
Alisema watumiaji wa tiba damu wapo wa makundi mbalimbali yakiwemo makundi ya akina mama wajawazito (kabla, wakati na baada ya kujifungua), kundi la majeruhi wa ajali mbalimbali, kundi la watoto, kundi la wagonjwa wa upasuaji na kundi la wagonjwa wa magonjwa wa kudumu kama vile seli mundo (sickle cell disease) na kansa mbalimbali hasa kansa ya damu. Makundi haya ni moja ya makundi ya wagonjwa wanaotumia tiba damu kwa kiwango kikubwa, hivyo uwepo wa damu muda wote katika benki zetu za damu ni suala la lazima ili kuimarisha afya na kulinda uhai wa maisha yao.
“Hivyo niiase jamii ione umuhimu wa kuchangia damu mara kwa mara, kwa kuwa na moyo wa kufanya hivyo kutawezesha benki zetu za damu kuwa na damu ya kutosha kuwahudumia wahitaji wanapojitokeza wakati wowote ili kuepuka kupambana na changamoto za utafutaji wa damu kwa dharura katika kuwahudumia wagonjwa wahitaji wa tiba damu wakati wote” Alisema ndugu Mtobu.
EmoticonEmoticon