ADPA WAKUTANA ARUSHA,WAKUBALIANA KUSIMAMIA MAUZO YA SOKO LA ALMASI DUNIANI.

July 28, 2022

 



Mwandishi wetu,Arusha 

Umoja wa baraza la mawaziri wa jumuiya ya nchi za Afrika zinazozalisha almasi (ADPA) umekubaliana kusimamia biashara ya madini aina ya almasi ili kuzinufaisha nchi wanachama.

Waziri wa madini nchini,Dotto Biteko amesema kwamba mkutano wa baraza la mawaziri kwa nchi zinazozalisha almasi umekutana jijini Arusha kwa lengo la kuidhinisha nyaraka muhimu za baraza hilo,kuteua sekretarieti sanjari na kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa na sauti moja katika kusimamia madini ya almasi.

Waziri Biteko amesisitiza kuwa wajumbe wa baraza hilo wataupitia upya mfumo wa umoja huo na kujifunza katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi barani Afrika ili yaweze kuwanufaisha waafrika.

amesema kuwa duniani kote madini ya almasi yana urasimu na mlolongo mpana hivyo mkutano huo utatoa fursa wajumbe kuchambua na kuangalia vigezo kwa baadhi ya nchi barani Afrika zilizopigwa marufuku kufanya biashara ya almasi duniani.

“Tutaupitia upya mfumo wa umoja wetu ikiwemo katiba na kuboresha miongozo mbalimbali katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi Barani Afrika “alisisitiza Biteko 

Tanzania ni mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa ADPA ambapo umoja huo unajumuisha nchi 18 barani Afrika ambapo nchi 12 wanachama na 6 ni waangalizi. 


Hata hivyo,Waziri Biteko amesema licha ya changamoto ya janga la UVIKO-19 Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mauzo ya madini aina ya almasi katika soko la dunia.

Waziri Biteko amesema kwamba baada ya janga la UVIKO-19 bei ya almasi duniani ilianguka  lakini kwa sasa almasi imepanda juu na kuifanya Tanzania kuendelea kufanya vizuri duniani.

Waziri Biteko amesema kuwa hivi karibuni kupitia mgodi wa almasi wa Mwadui uliopo mkoani Shinyanga serikal imeuza jiwe moja la almasi lenye kareti sita kwa thamani ya dola milioni 12 katika soko la dunia jambo ambalo linaashiria mafanikio makubwa kwa nchi.

“Huu uzalishaji haujawahi kutokea katika mgodi wetu wa Mwadui kwani tumeuza jiwe moja la almasi ya pink kwa thamani ya dola milioni kumi na mbili haya ni mafanikio makubwa sana kwa nchi yetu “alisema Biteko 

Waziri Biteko amesema kwamba pamoja na mgodi wa Mwadui kusimamisha uzalishaji kwa muda kutokana na ukarabati lakini kwa sasa serikali imeongeza hisa kutoka asilimia 25 mpaka 35 kama juhudi za kuongeza uzalishaji wa almasi hapa nchini.

Mwisho

.TUTAISHANGAZA DUNIA -TIMU YA JUMUIYA YA MADOLA

July 28, 2022


Na John Mapepele, Birmingham - Uingereza

Kocha Mkuu Timothy Kingu wa kikosi cha ndondi kinachoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola ambayo yanaanza rasmi leo Julai 28,2022 amemhakikishia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na watanzania wote kurejea na medali za ushindi kwenye mchezo huo kwa kuwa wamepata maandalizi ya kutosha.

Akizungumza katika kambi ya wachezaji hao jijini Birmingham, Uingereza amesema wachezaji wake wamepikwa vizuri na watapata hamasa ya kutosha tayari kwa ajili ya pambano lililopo mbele yao.

Aidha, amesema hamasa kubwa inayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri anayesimamia Michezo nchini, Mhe Mohamed Mchengerwa na wadau mbalimbali kwa sasa zinawafanya wawe na ali na nguvu zaidi ya kushindana kufa na kupona kwenye mashindano haya.

Hadi sasa, tayari Mabondia wawili wa Tanzania Yusuf Changarawe na Kassim Mbundwike wameingia robo fainali za mchezo ya Jumuiya ya Madola inayoanza rasmi leo jijini Birmingham, Uingereza.

Bondia wa tatu wa Tanzania, Alex Isinde sio tu ataanzia mzunguko wa kwanza bali pia atakuwa ndiye Mtanzania wa kwanza kutupa kete kwenye mashindano haya ya 48 ya nchi zilizopata kutawaliwa na Uingereza kesho Julai 29, 2022. 

Isinde atapambana na bondia kutoka Antigua & Barbuda aitwaye Alston Ryan. 

Endapo Isinde atashinda ataungana na wenzie katika robo fainali ambapo mshindi anabeba medali ya shaba.

Endapo wakishinda robo fainali wataingia nusu fainali ambako watawania kunyakua angalau medali za fedha.

Michezo ya Jumuiya ya Madola 2022 inazinduliwa rasmi leo saa mbili usiku kwa saa za huku (Tanzania iko mbele kwa saa mbili).

Tanzania itatupa tena kete zingine siku ya Jumamosi Julai 30, 2022 wakati wanariadha wanne wa mbio ndefu (Marathon) wanawake na wanaume wataingia kuchuana.

Wanariadha hao wa marathon ni Alphonce Simbu, Hamisi Misai, Jakline Sakilu na Failuna Matanga.

Kwenye michezo hiyo Tanzania inawakilishwa na wanariadha tisa, mabondia watatu, wacheza judo wawili, waogeleaji wawili na mnyanyua vitu vizito kwa walemavu (Para-Powerlifting) mmoja.

TANGA UWASA YATENGA MILIONI 900 KUPUNGUZA UPOTEVU WA MAJI

July 28, 2022
Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shabani wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Maji Cup yanayofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kombezi Jijini Tanga kushoto ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shilloo kulia ni  Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia usambazaji maji (ATAWAS) Constantine Chiwalo
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shiloo  akizungumza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shabani

 

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia usambazaji maji (ATAWAS) Constantine Chiwalo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo ya Maji Cup





Na Oscar Assenga,TANGA.



MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) katika mwaka wa fedha 2022/2023 wametenga milioni 990 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kuhakikisha wanapambana na upotevu wa maji.

Hayo yalisemwa  na Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shabani wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Maji Cup yanayofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kombezi Jijini Tanga.

Alisema fedha hiyo imetengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali zikazopelekea kupunguza upotevu wa maji ambapo mwaka jana ulikuwa wastani wa asilimi 30 kwa kutekeleza hayo hiyo miradi wanaimani watapunguza upotevu huo hadi kufikia asilimia 26 June 2023.

Alisema kazi ambazo wanazilenga kuzifanya ni kuboresha miundombinu kwa ajili ya kuzibiti na kupunguza upotevu wa maji kutoka kwenye mabomba na watanunua na kufunga mita za malipo kabla hizo mita ni za aina yake na hivyo itakuwa mamlaka ya maji ya kwanza kuonyesha aina hiyo ya mita.



“Mita hizi tunatarajia tutaanza kuzifunga mwezi huu uzuri mita hizi kama kuna uvujaji mbele ya mita mteja anapata ujumbe kuna matumizi yanafanyika hebu fuatilia agizo hilo ni la wizara na sisi tunatekeleza kwa sababu tunataka kufunga mita ambazo ni rafiki kwa mtumiaji hiyo ni aina rafiki kwa sababu ina mjali mteja”Alisema



Kaimu Mkurugenzi huyo alisema wamekuwa wakipokea malalamiko bili kubwa na moja ya chanzo ni maji kuvunja mbele ya mita hivyo hilo litakwenda kutatua hilo tatizo ikiwemo kuendelea kuelimisha jamii juu ya udhibiti wa upotevu wa maji na utoaji wa taarifa kwa mamlaka.



“Tunamshukuru Rais kutoa fedha zilizowezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maji inayolenga kuondoa kero ya maji nchini na nyengine nga imeshaleta mabadiliko makubwa ya utapatikanaji wa huduma ya maji nchini ikiwemo Jiji la Tanga ambapo kwa sasa imefikia asiimia 97”Alisema



Hata hivyo alisema Serikali itoa bilioni 13.31kwa ajili ya kujenga miradi ya maji kuhakikisha wananchi wa Jiji la Tanga wanapata huduma ya maji safi na salama.

Alisema pia wamepenga kutanua mtambo wa kusafisha maji eneo la Mowe ambapo wametenga Bilioni 9.1 na kwa sasa unaendelea na umefikia asilimia 62.

“Lakini pia tumeendeleza mtandao wa mabomba kilimota 17.6 maeneo ya Kichangani,Pongwe,Masiwani na Neema huu ni mradi wa kukabiliana na ugonjwa wa Uviko na umekamilika asilimia 100 ulikuwa na thamani milioni 500”Alisema

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema licha ya hivyo serikali imewezesha fedha kujenga mradi wa maji kufikisha huduma maeneo ya Kibafuta,Mleni ,ndaoya,mpirani na chongoleani na kata ya chongoleani ni eneo pekee la Jiji la Tanga ambalo lilikuwa halina mtandao wa huduma ya maji sasa miundombinu imefika na wananchi na wameanza kupata huduma hiyo ya maji.

“Mradi hu wa kupelekea maji Chongoleani una thamani ya Milioni 918 na utekelezaji mradi umefikia asilimi 90 lakini pia kuna mradi wa kulaza bomba kubwa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo ”alisema


 

Alieleza hiyo inatokana na wananchi wa eneo la Chongoleani kupata maji kwa mgawo na serikali imetoa bilioni 2.7 kwa ajili ya kulaza bomba kubwa kutoka eneo la Amboni mpaka Chongoleani ili kuhakikisha wanapata maji muda wote.

 

Mwisho.

 

WAZIRI MCHENGERWA AITEMBELEA TIMU YA JUMUIYA YA MADOLA,AIFUNDA

July 28, 2022

 


Na John Mapepele, Birmingham


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa ameitembelea timu ya wachezaji wa Tanzania inayoshiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola   Birmingham nchini Uingereza na kuitaka kupambana kufa na kupona ili kurejea na medali.

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Julai 27, 2022 kwenye kambi ya timu hiyo huku akisisitiza kuwa watanzania wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan wana matumaini makubwa na timu hiyo hivyo hawana budi kulinda heshima kubwa waliyopewa na taifa kwa ujumla.

"Nawaomba tangulizeni uzalendo ili tuweze kushinda, hii ni vita  tunahitaji kupambana bila kujali idadi yetu wala kitu chochote. Tutashinda." Amesisitiza Mhe. Mchengerwa


Aidha,  amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuinua  na kuendeleza michezo kwa kuwa michezo ni chanzo. Ha ajira na uchumi kwa taifa

" kwa kutambua hilo ndiyo maana kwa mara ya kwanza Serikali  imeamua kutoa fedha nyingi kwa wachezaji watakaopata medali za dhahabu dola za kimarekani 10,000, shaba 7500 na fedha 5000 bado zawadi za jumla" amesisitiza  Mhe. Mchengerwa.

Pia ametumia tukio hilo kutoa pongezi kwa timu ya wanaume na wanawake ya KABBADI kwa kufuzu kuingia kwenye mashindano ya kombe la Dunia yatakayofanyika Oktoba mwaka huu nchini India.

Mhe Mchengerwa ameongozana na Mhe. Musa Sima Mjumbe wa Kamati ya Bunge inayosimamia wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na ndugu Saidi Yakubu Naibu Katibu Mkuu.

WAZIRI MCHENGERWA AZIPONGEZA TIMU ZA KABBADI KUFUZU KOMBE LA DUNIA

July 27, 2022

 

 

HOMA YA MGUNDA ISIWE KIKWAZO CHA KUTOKULA NYAMA

July 27, 2022

 Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma na kuwaasa watanzania kuwa ugonjwa wa Homa ya Mgunda usiwe kikwazo kwao kula nyama bali wapate nyama kwenye machinjio rasmi ambapo nyama hizo zinakaguliwa na mtaalamu wa mifugo kutoka serikalini. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Daniel Mushi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma na kuwashauri watanzania wapate nyama kwenye machinjio rasmi na ipikwe iive vyema kufikia nyuzi joto sabini (70) kabla ya kula ili kuua vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda pamoja na kuhakikisha nyama wanayokula kwenye maeneo ya starehe inachomwa vizuri na kukaushwa damu yake. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga (kulia) akiwa na Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Daniel Mushi wakati walipozungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kutoa ufafanuzi juu ya ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa nyama inayopatikana kutoka kwenye mifugo hapa nchini, kutokana na uwepo wa baadhi ya taarifa zisizo sahihi juu ya uwepo wa ugonjwa huo na ulaji wa nyama. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na. Edward Kondela



Serikali imesema ugonjwa wa Homa ya Mgunda usiwe kikwazo cha watanzania kutokula nyama na kwamba asilimia tisini ya nyama inayopitia kwenye machinjio rasmi iko salama.

Akizungumza jijini Dodoma (27.07.2022) kupitia vyombo mbalimbali vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema, nyama ya mnyama anayechinjwa kwenye machinjio rasmi huwa inakaguliwa na mtaalamu wa mifugo wa serikali kabla ya kwenda sokoni ili kuepusha madhara yoyote kwa binadamu.

Prof. Nonga amebainisha kuwa kutokana na utafiti uliofanywa umebaini kuwa mnyama ambaye ameathirika na vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda akitolea mfano wa ng’ombe, nyama yake inakuwa na rangi ya njano hivyo ni rahisi kwa mtaalam wa mifugo kubaini nyama hiyo machinjioni na kutoruhusu kupelekwa sokoni.

“Kuchinja mifugo kwenye machinjio na nyama ikaguliwe na daktari au mtaalamu wa mifugo wa serikali kwa kuwa tushaona ng’ombe akipata shida ya Homa ya Mgunda, nyama yake inakuwa na rangi ya njano hivyo mtaalam atagundua kuwa haifai kwa matumizi ya binadamu, hivyo watanzania watakuwa salama.” Amesema Prof. Nonga

Ameongeza kuwa njia nyingine ya watanzania kujikinga na ugonjwa wa Homa ya Mgunda ni kuhakikisha nyama inapikwa vyema na kuiva ili kuua vimelea vya ugonjwa huo ambavyo vinaishi kwenye majimaji ya mnyama ambaye ameathirika, ukiwemo mkojo na kinyesi chake.

Aidha, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amewataka watanzania kutokula nyama ya wanyama wasiyo rasmi kwenye chakula akiwemo panya kwa kuwa amebainika kuwa ni moja ya wanyama ambao wanahusishwa kwa kiasi kikubwa kubeba vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda na magonjwa mengine.

Amefafanua kuwa ulaji wa nyama ni muhimu katika mwili wa binadamu kwa kuwa ni chanzo cha Protein katika daraja la kwanza ikiwa ni pamoja na kinga mwilini, hivyo watanzania wanatakiwa kula nyama iliyo rasmi katika kundi la chakula, kununua nyama iliyokaguliwa na mtaalamu wa mifugo wa serikali kwenye machinjio rasmi pamoja na kuipika nyama hiyo vyema na kuiva ili kuua vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda pamoja na magonjwa mengine.

Pia, amewaasa wafugaji kuhakikisha wanachanja mifugo yao dhidi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa Homa ya Mgunda ambao umekuwepo kwa siku nyingi lakini umeanza kuonesha athari kwa binadamu.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Daniel Mushi amewatahadharisha watanzania wanaokula nyama kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo ya starehe kuhakikisha nyama imechomwa na kukauka vizuri na kutokuwa na damu kwa kuwa ikipikwa vizuri hakuna sababu ya kuogopa ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa sababu vimelea vyake vinakufa kwenye mapishi yanayofikia nyuzi joto sabini (70).

Dkt. Mushi amewaasa pia watanzania kununua nyama kwenye maduka yaliyosajiliwa na kukaguliwa ambapo nyama iliyokaguliwa inakuwa na mhuri kwenye mguu wa nyuma wa mnyama na kuwataka kuacha kula nyama kutoka kwenye machinjio yasiyo rasmi yasiyoeleweka au nyama inayopatikana mitaani kwa bei nafuu kwa kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.

Ameongeza kuwa ni wajibu kwa watoa huduma kwenye maduka ya nyama kutakiwa kupimwa afya zao kila baada ya miezi sita ili wasiwe chanzo cha maradhi mengine kwa walaji wa nyama wanazouza.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Bodi ya Nyama Tanzania zimelazimika kutoa taarifa juu ya ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa nyama inayopatikana kutoka kwenye mifugo hapa nchini, kutokana na uwepo wa baadhi ya taarifa zisizo sahihi juu ya uwepo wa ugonjwa huo na ulaji wa nyama.

ZAIDI YA WATANZANIA MILIONI 61 KUHESABIWA KWENYE SENSA YA WATU NA MAKAZI MWAKA HUU

July 26, 2022
 Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anna Makinda akizungumza wakati wa kikao cha viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Tanga,Serikali wakiwemo wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akifuatiliwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Pili Manyema na Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandiliwa

MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza wakati wa kikao hicho kushoto ni Kamisa wa Sensa ya Watu na Makazi nchini Anna Makinda na kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Pili Manyema akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa

MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza wakati wa kikao hicho kushoto ni Kamisa wa Sensa ya Watu na Makazi nchini Anna Makinda na kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Pili Manyema akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa



 Na Oscar Assenga, TANGA.

ZAIDI ya watanzania Milioni 61 wanakadiriwa kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakalofanyika Agosti 23 mwaka huu hapa nchini.

Hayo yalisemwa na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Anna Makinda wakati wa kikao cha viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Tanga,Serikali wakiwemo wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri.

Alisema Sensa ni kitu muhimu kinachoipa Serikali ubora wa kufanya kazi zake na ya mwaka huu itakuwa tofauti kabisa ndio maana wakadiria watanzania milioni 61 hadi 64 kutokana na uzazi walioupata mwaka 2012 walikuwa wakiongeza kwa asilimia 2.9.

Alisema suala la Sensa ni takwa la kisheria na ni ustarabu wa kuendesha serikali mbalimbali ulimwenguni kutokana na kwamba unapokuwa na watu basi uwajue ili uweze kupanga mipango yako vizuri.

“Lengo la Sensa ni kujua idadi ya watanzania kama ham hesabiani itakuwa ni fujo sana kuweza kuendesha nchi hivyo ni jambo muhimu kama kiongozi lazima ujue idadi ya watu wako”Alisema

Alisema kwamba sensa ya mwaka huu itakwenda kidigitali na mpaka sasa sasa makarani waliotenga maeneo wanayo kabisa kwamba kitongoji hiki kina nyumba ngapi na hali gani na kitu gani.

Aidha alisema kutokana na hilo hakuna namna karani wa Sensa anaweza kuruka nyuma ataonekana toka Dodoma na wamechukua picha za Satelite kila nyuma inaonekana kwa maana wanahesabu na majengo pia.

Kamisaa huyo alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana kuwasiliana na watu kwa karibu sana hivyo ni muhimu wakatumia nafasi zao kuhamasisha zoezi hilo kwenye madhehebu yao.

“Viongozi wa dini ni mwakilishi wa Mungu ,watu wanawasikilizeni mkisema hawafanyi ubishi na viongozi wa mila pia watu wana watii sana hata waganga wa kienyeji wanaheshimika kama mtu anaweza kulala huko kugaragara hao watu wanaaminika kwa asilimia kubwa”Alisema Kamisaa.

Awali akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alisema watu ambao watataka kuhujumu zoezi la Sensa watatumia sheria kali dhidi yao kwa sababu watakuwa hawana nia ya maendeleo.

Alisema suala la sensa ya watu na makazi ni jambo muhimu sana hasa kwenye kupanga maendeleo ya nchi na mgao wa rasilimali kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya na ujenzi wa miundombinu na nyengine zote.

Malima alisema huko nyuma zoezi hilo lilikuwa likipata shida kidogo kutokana na kutokufahamu kwamba viongozi wa dini wanasikilizwa sana kwenye maeneo yao hivyo hakikisheni mnalihamasiha.



Alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika madhehebu yao kulihamasisha suala hilo ili kuhakikisha waumini wao wanashiriki kwenye zoezi hilo la kuhesabiwa kutokana na kwamba kila mtu anamuamini kiongozi wa kiroho.



Mwisho.

WAZIRI MCHENGERWA AONGOZA KIKAO CHA UJUMBE WA TANZANIA BIRMINGHAM UINGEREZA

July 25, 2022

 


















Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe,  Mohammed Mchengerwa  ameongoza kikao cha maandalizi ya ujumbe wa Tanzania katika kikao cha Mawaziri wa Michezo wa Jumuiya ya Madola kitakachoanza leo Julai 26 mjini Birmingham, Uingereza. 


Kikao hicho ni maandakizi mahususi kabla ya uzinduzi rasmi wa mashindano ya michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka huu yanayofanyika nchini Uingereza huku Tanzania ikiwa imeshiriki katika michezo hiyo.

Katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza Serikali imetoa  motisha kubwa kwa wachezaji watakaofanya vizuri na kurejea na tuzo nchini.

Mhe. Mchengerwa amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha   michezo inatumika kikakamilifu kuitangaza Tanzania kimataifa.

Aidha, amesema michezo ni ajira na uchumi mkubwa ambapo amesisitiza wachezaji wote kuwa wazalendo kujituma kufa na kupona kwa ajili ya taifa la Tanzania.

Amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuleta mapinduzi  makubwa kwenye sekta za michezo katika kipindi kifupi iliyopo madarakani.

Miongoni mwa motisha hizo amesema  Serikali itatoa kiasi cha  dola  10,000 za kimarekani kwa mchezaji atakayerejea na medali ya dhahabu, dola 7000 kwa medali ya Shaba na dola 5000 kwa medali ya fedha.

 Kikao hicho kimehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt, Asha-Rose Migiro, Mhe. Mussa Sima ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo Ndugu Saidi Yakubu pamoja na wajumbe kutoka Tanzania.

VIFARANGA VYA KUKU KUTOKA NJE YA NCHI MWISHO JULAI 30

July 23, 2022



Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akizungumza kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma na kuweka wazi kuwa baada ya tarehe 30 mwezi huu, hakuna vifaranga vya kuku vitakavyoingizwa hapa nchini kutoka nje ya nchi na kwamba serikali haitoi tena vibali vya kuingiza vifaranga hivyo ili kuzuia ugonjwa mafua ya ndege na kulinda wazalishaji wa vifaranga wa ndani ya nchi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Stephen Michael ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko akizungumza kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma ambapo amesema katika Mpango Kabambe wa Sekta ya Mifugo wa Mwaka 2016 umefanya tathmini na kuainisha kuwa hadi kufikia Mwaka 2031 kutakuwa na upungufu wa nyama kwa tani milioni 1.8 hivyo tasnia ya kuku ni rahisi ikitiliwa mkazo itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa nyama nchini. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo Bw. Evance Ntiyalundura akiwa kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku jijini Dodoma ambapo amefafanua hatua mbalimbali katika kukuza tasnia hiyo ikiwemo ya kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na wadau wa tasnia. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga, akiwa mmoja wa washiriki katika kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma na kuelezea umuhimu wa wadau kujisajili kwenye mfumo ili kutambulika kisheria na namna serikali inavyotoa vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo kikiwemo cha kuku. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rweguza akifafanua umuhimu wa matumizi ya vyakula bora vya mifugo hususan vya kuku na kuwakumbusha wazalishaji wa vyakula hivyo kutumia maabara ya Wakala ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuhakiki ubora wa vyakula wakati aliposhiriki kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Dkt. Daniel Mushi akitolea ufafanuzi ombi la wafugaji wa kuku kuwepo kwa machinjio ya kuku kila wilaya ili kuzuia uuzwaji holela wa kuku na kuwepo kwa bei elekezi ya kuku sokoni, wakati aliposhiriki kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)



Katibu wa Chama cha Wadau wa Kuku Tanzania (PAT) Bw. Manase Mrindwa akielezea changamoto za chakula cha kuku kuwa kumetokea ongezeko la bei ya chakula cha kuku hadi kufikia Shilingi Elfu 80 kwa mfuko mmoja kwa mwezi wa Julai kutokana na ongezeko la bei ya mahindi na mashudu ya soya kwenye soko la Tanzania pamoja na kuelezea uwepo wa uhaba wa vifaranga, wakati akisoma taarifa ya chama hicho kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Muonekano wa washiriki katika kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo kimejumuisha menejimenti ya wizara Sekta ya Mifugo, wazalishaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na wafugaji wa kuku ambapo wametoa maoni mbalimbali ya namna ya kuboresha tasnia hiyo na kuomba kuwepo kwa vikao vya namna hiyo mara kwa mara lengo likiwa ni kukuza tasnia. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)





Na. Edward Kondela




Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema baada ya tarehe 30 mwezi huu, hakuna vifaranga vya kuku vitakavyoingizwa hapa nchini na kwamba serikali haitoi tena vibali vya kuingiza vifaranga hivyo.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (22.07.2022) jijini Dodoma wakati wa kikao cha wizara na wadau wa tasnia ya kuku, kujadili namna ya kukuza tasnia hiyo ambapo lengo la hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria ya mwaka 2006 ambapo serikali imekuwa ikizuia uingizaji wa vifaranga nchini kutoka nje ya nchi ili kudhibiti ugonjwa wa mafua ya ndege kwa mifugo jamii ya ndege na kulinda wazalishaji wa kuku ndani ya nchi.

Akizungumza wakati akifunga kikao hicho kilichojadili ajenda mbalimbali zikiwemo za upatikanaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na bei ya kuku sokoni, Mhe. Ulega amesema ni mategemeo kuwa serikali haitaona vifaranga vinaingizwa nchini kutoka nje ya nchi na kutaka kuwepo kwa mfumo wa taarifa zinazohusu wazalishaji wa vifaranga vya kuku kuanzia wazalishaji wakubwa hadi wadogo ambao wamesajiliwa na kutoa taarifa serikalini ili kuiwezesha kujua kiwango cha uzalishaji na kuwa na takwimu sahihi juu ya mahitaji ya vifaranga nchini.

“Ni mategemeo yetu ni kutokuona baada ya tarehe 30 mtu anaingiza vifaranga hapa nchini kutoka mahali popote pale, jambo la pili kuwepo na mfumo ambao utasaidia serikali kujua ni kiasi gani cha uzalishaji vifaranga ndani ya nchi yetu ili kujipima uwezo wetu na mahitaji yetu ndani ya nchi.” Amesema Mhe. Ulega

Awali Naibu Waziri Ulega akizungumza wakati akifungua kikao hicho cha wizara na wadau wa tasnia ya kuku amesema tasnia hiyo imekua kwa kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na kuwepo kwa soko linalotokana na ongezeko la watu na kipato, ongezeko la uwekezaji na uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji katika tasnia ya kuku, urahisi wa kufuga kuku na uwezekano mkubwa wa kuwamiliki kuliko wanyama wakubwa.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Stephen Michael akizungumza kwenye kikao hicho amesema kutokana na umuhimu wa tasnia ya kuku katika Mpango Kabambe wa Sekta ya Mifugo wa Mwaka 2016 umefanya tathmini na kubainisha kuwa hadi kufikia Mwaka 2031 kutakuwa na upungufu wa nyama kwa tani milioni 1.8 hivyo tasnia ya kuku ni rahisi ikitiliwa mkazo itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa nyama nchini.

Bw. Michael ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema ufugaji wa kuku ni njia rahisi na ambayo haihitaji maeneo makubwa na miundombinu mingi tofauti na mifugo mingine hivyo kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kimeunganisha wadau wa tasnia hiyo pamoja na kutatua changamoto zilizopo kwa kuzingatia uwepo wa taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo kwa vijana na akina mama na vikundi mbalimbali ambao wengi wamejizatiti katika biashara ya kuku.

Naye Katibu wa Chama cha Wadau wa Kuku Tanzania (PAT) Bw. Manase Mrindwa amebainisha changamoto za chakula cha kuku kuwa kimefikia hadi Shilingi Elfu 80 kwa mfuko mmoja kwa mwezi wa Julai ambapo kunatokana hasa na ongezeko la bei ya mahindi na mashudu ya soya kwenye soko la Tanzania.

Bw. Mrindwa amebainisha pia changamoto ya kutokea kwa uhaba wa vifaranga kwa wakati fulani wa mwaka, huku mitaani bado viko vifaranga visivyo bora ambavyo vinawafikia wafugaji hususan wafugaji wadogo.

Kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kimejumuisha menejimenti ya wizara Sekta ya Mifugo, wazalishaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na wafugaji wa kuku ambapo wametoa maoni mbalimbali ya namna ya kuboresha tasnia hiyo na kuomba kuwepo kwa vikao vya namna hiyo mara kwa mara lengo likiwa ni kukuza tasnia hiyo kwa kuirasimisha na kuwepo kwa machinjio maalum kwa ajili ya kuku na bei elekezi ya kuku sokoni.

Mwisho

WAZIRI MCHENGERWA AMWAGA VIFAA VYA MICHEZO SHULE ZOTE WILAYA YA RUFIJI,AANZISHA LIGI YA SENSA

July 18, 2022

 

 





Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Rufiji.  Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa ametoa vifaa vya michezo kwa shule zote za msingi na Sekondari na wanafunzi wanamichezo wote  wanaoshiriki kwenye mashindano ya michezo kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Mashindano  ya Shule za Sekondari (UMISSETA) kwa mwaka 2022 Wilaya ya Rufiji.


Mhe. Mchengerwa amekabidhi  vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Julai 17, 2022 kwenye  shule ya Sekondari ya Ikwiriri   Wilaya ya Rufiji ambapo amesema ameamua  kufadhili vifaa hivyo katika Wilaya ya Rufiji ili kuiendeleza michezo kwa kuwa michezo ni biashara  na ajira kubwa  kwa vijana.


“Nimeamua kusaidia vifaa hivi kwakuwa natambua  kwa sasa michezo ni miongoni mwa chanzo cha ajira na biashara kubwa duniani hivyo ni vema kufanya michezo kwa umakini mkubwa ili kujipatia ajira” amefafanua


Amewataka wachezaji hao kuwa na nidhamu na kujituma kwa kufanya mazoezi ili waweze kushinda kwenye  mashindano mbalimbali.

“Nendeni mkajitume, michezo ni ajira na  furaha wasikilizeni walimu wenu,  hata shuleni  mtafanya  vizuri”amesisitiza Mhe. Mchengerwa.

Aidha amesema dhamila ya Serikali kwa sasa  ni kuendeleza michezo ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazofanya kwenye michezo  katika kipindi kifupi cha utawala wake ambazo zimeleta  mapinduzi makubwa kwenye sekta  hiyo.

Vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya milioni 23 ambazo zimenunua zaidi ya jezi seti 200, trakisuti pea 100, kofia 200 na mipira 100.

Pia amefadhili Ligi ya mpira wa miguu ya   sensa katika Wilaya ya Rufiji ambapo ametoa seti 6 za jezi kwa timu sita na  mipira  12 kwa ajili ya mashindano  hayo.


Amesema lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha  wananchi  kushiriki kuhesabiwa  kwenye sensa ya kitaifa  yam waka huu  kwa manufaa mapana ya wananchi wa Rufiji na Taifa kwa ujumla.


Aidha, amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Rufiji na watanzania wote kujitokeza kwa wingi Agosti 23, mwaka huu kuhesabiwa kwenye zoezi la sensa kitaifa.

Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Rufiji amemshukuru Mhe. Mchengerwa  kwa jitihada  zake  na mchango wake kwenye sekta ya michezo ambapo amemhakikishia kuwa michango anayotoa itatumika vizuri ili  kupata matokeo chanya.