Mkurugenzi
wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma na
kuwaasa watanzania kuwa ugonjwa wa Homa ya Mgunda usiwe kikwazo kwao
kula nyama bali wapate nyama kwenye machinjio rasmi ambapo nyama hizo
zinakaguliwa na mtaalamu wa mifugo kutoka serikalini. (Picha na Edward
Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Msajili
wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Daniel Mushi akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) jijini Dodoma na kuwashauri watanzania wapate
nyama kwenye machinjio rasmi na ipikwe iive vyema kufikia nyuzi joto
sabini (70) kabla ya kula ili kuua vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda
pamoja na kuhakikisha nyama wanayokula kwenye maeneo ya starehe
inachomwa vizuri na kukaushwa damu yake. (Picha na Edward Kondela, Afisa
Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkurugenzi
wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga
(kulia) akiwa na Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Daniel Mushi
wakati walipozungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kutoa
ufafanuzi juu ya ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa nyama inayopatikana
kutoka kwenye mifugo hapa nchini, kutokana na uwepo wa baadhi ya taarifa
zisizo sahihi juu ya uwepo wa ugonjwa huo na ulaji wa nyama. (Picha na
Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Na. Edward Kondela
Serikali imesema
ugonjwa wa Homa ya Mgunda usiwe kikwazo cha watanzania kutokula nyama na
kwamba asilimia tisini ya nyama inayopitia kwenye machinjio rasmi iko
salama.
Akizungumza jijini Dodoma (27.07.2022) kupitia vyombo
mbalimbali vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema, nyama ya mnyama anayechinjwa
kwenye machinjio rasmi huwa inakaguliwa na mtaalamu wa mifugo wa
serikali kabla ya kwenda sokoni ili kuepusha madhara yoyote kwa
binadamu.
Prof. Nonga amebainisha kuwa kutokana na utafiti
uliofanywa umebaini kuwa mnyama ambaye ameathirika na vimelea vya
ugonjwa wa Homa ya Mgunda akitolea mfano wa ng’ombe, nyama yake inakuwa
na rangi ya njano hivyo ni rahisi kwa mtaalam wa mifugo kubaini nyama
hiyo machinjioni na kutoruhusu kupelekwa sokoni.
“Kuchinja
mifugo kwenye machinjio na nyama ikaguliwe na daktari au mtaalamu wa
mifugo wa serikali kwa kuwa tushaona ng’ombe akipata shida ya Homa ya
Mgunda, nyama yake inakuwa na rangi ya njano hivyo mtaalam atagundua
kuwa haifai kwa matumizi ya binadamu, hivyo watanzania watakuwa salama.”
Amesema Prof. Nonga
Ameongeza kuwa njia nyingine ya watanzania
kujikinga na ugonjwa wa Homa ya Mgunda ni kuhakikisha nyama inapikwa
vyema na kuiva ili kuua vimelea vya ugonjwa huo ambavyo vinaishi kwenye
majimaji ya mnyama ambaye ameathirika, ukiwemo mkojo na kinyesi chake.
Aidha,
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.
Hezron Nonga amewataka watanzania kutokula nyama ya wanyama wasiyo rasmi
kwenye chakula akiwemo panya kwa kuwa amebainika kuwa ni moja ya
wanyama ambao wanahusishwa kwa kiasi kikubwa kubeba vimelea vya ugonjwa
wa Homa ya Mgunda na magonjwa mengine.
Amefafanua kuwa ulaji wa
nyama ni muhimu katika mwili wa binadamu kwa kuwa ni chanzo cha Protein
katika daraja la kwanza ikiwa ni pamoja na kinga mwilini, hivyo
watanzania wanatakiwa kula nyama iliyo rasmi katika kundi la chakula,
kununua nyama iliyokaguliwa na mtaalamu wa mifugo wa serikali kwenye
machinjio rasmi pamoja na kuipika nyama hiyo vyema na kuiva ili kuua
vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda pamoja na magonjwa mengine.
Pia,
amewaasa wafugaji kuhakikisha wanachanja mifugo yao dhidi ya magonjwa
mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa Homa ya Mgunda ambao umekuwepo kwa siku
nyingi lakini umeanza kuonesha athari kwa binadamu.
Kwa upande
wake Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Daniel Mushi
amewatahadharisha watanzania wanaokula nyama kwenye maeneo mbalimbali
yakiwemo ya starehe kuhakikisha nyama imechomwa na kukauka vizuri na
kutokuwa na damu kwa kuwa ikipikwa vizuri hakuna sababu ya kuogopa
ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa sababu vimelea vyake vinakufa kwenye
mapishi yanayofikia nyuzi joto sabini (70).
Dkt. Mushi amewaasa
pia watanzania kununua nyama kwenye maduka yaliyosajiliwa na kukaguliwa
ambapo nyama iliyokaguliwa inakuwa na mhuri kwenye mguu wa nyuma wa
mnyama na kuwataka kuacha kula nyama kutoka kwenye machinjio yasiyo
rasmi yasiyoeleweka au nyama inayopatikana mitaani kwa bei nafuu kwa
kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.
Ameongeza kuwa ni wajibu
kwa watoa huduma kwenye maduka ya nyama kutakiwa kupimwa afya zao kila
baada ya miezi sita ili wasiwe chanzo cha maradhi mengine kwa walaji wa
nyama wanazouza.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Bodi ya Nyama
Tanzania zimelazimika kutoa taarifa juu ya ugonjwa wa Homa ya Mgunda kwa
nyama inayopatikana kutoka kwenye mifugo hapa nchini, kutokana na uwepo
wa baadhi ya taarifa zisizo sahihi juu ya uwepo wa ugonjwa huo na ulaji
wa nyama.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon