Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (mwenye miwani) akishuhudia utiaji saini wa hati ya makabidhiano ya Kiwanda cha nyama cha Shinyanga. Hati hiyo zilisainiwa na Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba(aliyekaa upande wa kushoto) kutoka Hazina kwa upande wa Serikali na Balozi Fouad Mustafa (aliyeinama upande wa kulia) kwa upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group aliyemwakilisha mmiliki wa Kampuni hiyo bwana Ali Saeed Juma Albwardy.
Hati ya kiwanda cha nyama cha Shinyanga iliyorejeshwa Serikalini na Kampuni ya Albwardy Investment Group baada ya kuuziwa kinyemela na kampuni ya Tripple S Beef kinyume na mkataba iliyoingia na Serikali, baada ya kampuni hiyo kushindwa kukiendesha kiwanda kwa miaka 11 tangu kilipokabidhiwa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (aliyekaa mwenye miwani) akishuhudia ubadilishanaji wa hati ya makabidhiano ya Kiwanda cha nyama cha Shinyanga.Kushoto ni Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina aliyeiwakilisha Serikali na kulia ni Balozi Fouad Mustafa aliyewakilisha upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group
-Ni baada ya Waziri Mpina kutoa siku saba tu kuirejesha
Na John Mapepele, Dar es Salaam
Kampuni ya Albwardy Investment Group imerejesha Serikalini hati ya kiwanda cha nyama cha Shinyanga na eneo la kupumzishia mifugo la kiwanda hicho iliyouziwa kinyemela na kampuni ya Triple S Beef Limited kutokana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kutoa siku saba kwa wawekezaji Triple S Beef kusalimisha hati hizo kwa kushindwa kukiendeleza kwa miaka 11.
Akizungumza mara baada ya kusaini hati za makabidhiano ya hati hizo ofisini kwake jana, Waziri Mpina alitoa siku 14 kwa Salim Said Seif ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Tripple S Beef kujisalimisha Serikalini kwa kuvunja mkataba na serikali ambao ulimtaka kutommilikisha mwekezaji mwingine.
Hati hiyo zilisainiwa na Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina kwa upande wa Serikali na Balozi Fouad Mustafa kwa upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group aliyemwakilisha mmiliki wa Kampuni hiyo bwana Ali Saeed Juma Albwardy.
Waziri Mpina alisema Kampuni ya Tripple S Beef ilinunua kiwanda hicho kwa shilingi milioni 63 tu mwaka 2007 na kukiza kinyemela kwa shilingi bilioni 8 kwa Kampuni ya Albwardy Investment Group mwaka 2015 kwa mujibu wa maelezo ya mwakilishi wa kampuni hiyo, balozi Fouad Mustafa.
Aidha alisema kiwanda hicho kilijengwa kwa bilioni 8.2 na kina ukubwa wa eneo la hekta 32 huku likiwa na ziada ya eneo lenye hekta 444 zakuhifadhia mifugo.
Aidha Mpina alisema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuvifufua viwanda vyote vya nyama nchini na kuvitangaza kwa wawekezaji makini ili waweze kuwekeza ili mifugo iliyopo iweze kupata soko la uhakika na viwanda vilipe kodi za serikali hatimaye kuliingizia taifa mapato.
“Tunaposema Serikali ya awamu hii ni ya viwanda tuna maanisha kwa vitendo na kuhakikisha viwanda vyote vinafanya kazi katika kiwango kinachositahili ili kujenga uchumi wa nchi yetu” alisistiza Mpina
Aliongeza kuwakwa kuwa hati za kiwanda cha Shinyanga zimekabidhiwa leo zabuni itatangazwa hivi karibuni ya kumpata mwekezaji mahiri, pamoja na kiwanda hicho viwanda vingine vitakavyotangazwa kupata mwekezaji mahiri ni pamoja na kiwanda cha nyama Mbeya na kiwanda cha Ngozi cha Mwanza.
Alisema Serikali itavitangaza viwanda hivyo pamoja kuvitengea maeneo makubwa ya kuhifadhia mifugo kabla ya kuichinjwa ili kuinua ubora na thamani ya nyama katika masoko ya kimataifa.
Akitoa taarifa ya Umilikishwaji wa kiwanda hicho, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina alisema kiwanda kilianza ujenzi wake mwaka 1975 na kwamba kimegharimu dola za kimarekani milioni 3.5 na kilijengwa na Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Alisema mwaka 2007 kiwanda hicho kilibinafsishwa kwa mwekezaji Tripple S Beef Limited lakini kutoka na matatizo ya uendeshaji kiwanda hicho kilifungwa mwaka 2017 na kukabidhiwa kwa Serikali.
Awali Waziri Mpina alipofanya ziara ya kushitukiza hivi karibuni katika kiwanda cha nyama cha Shinyanga aliagiza kwamba ifikapo Juni 30 mwaka huu kiwanda hicho kiwe kimempata mwekezaji ambaye ataanza kazi mara moja ya uchinjaji ili kutoa ajira na kuliingizia taifa mapato.
Alitoa siku saba kwa wawekezaji waliokuwa wanaendesha kiwanda hicho kusalimilisha hati za kiwanda na eneo mara mmoja ili Serikali iweze kufanya taratibu za kufufua kiwanda hicho.
Aidha amemuagiza Msajili wa Hazina kuanza uhakiki wa mali zote za kiwanda hicho baada ya kubainika wizi uliokithiri katika kiwanda hicho.
Pia Mpina ameamuru mmliki wa Kampuni inayolinda kiwanda hicho kukamatwa mara moja na kufikishwa katika mikono ya sheria kwa ajili ya kujibu mashitaka wa wizi wa mali za kiwanda hicho ambapo alimtaka Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kuanzia sasa kiwanda hicho kilindwe na vyombo vya Serikali badala ya makampuni binafsi.