Ndugu Wawakilishi wa vyombo vya habari, nimewaiteni leo hii ili niwape taarifa fupi kuhusu malipo ya madai
ya malimbikizo ya mishahara kwa Watumimishi wa umma waliokuwa na madai
ili muweze kuufikishia umma wa Watanzania.
Serikali kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara (Human
Capital Management Information System – HCMIS) kufikia tarehe 01 Julai
2017 ilikuwa na madai ya malimbikizo ya mishahara yenye jumla ya shilingi
127,605,128,872.81 kwa watumishi 82,111 Wakiwemo walimu 53,925 waliokuwa
wanadai shilingi 53,940,514,677.23 sawa na asilimia 42.27 ya madai
yote, na wasiokuwa walimu 28,186 waliokuwa wanadai jumla
ya shilingi 73,664,614,195.58 sawa na asilimia 57.73 ya madai yote.
Madai haya yalikuwa ya muda mrefu mengine yakiwa ya kuanzia mwaka 2005
hadi mwaka 2017
Madai haya yalijumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara
kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa vyeo
na kuchelewa kurekebishiwa mishahara.
MATOKEO YA UHAKIKI WA MADAI YA SHILINGI BILIONI 127,605,128,872.81 KWA WATUMISHI
82,111
- Madai ya watumishi 27,389 kati 82,111 yenye jumla ya shilingi 43,393,976,807.23 ikiwa ni asilimia 34 ya madai yote ya shilingi bilioni 127,605,128,872.81 yaliyohakikiwa yameonekana ni sahihi na yanastahili kulipwa bila marekebisho.
- Madai yanayostahili kulipwa yanajumuisha shilingi bilioni 16.25 kwa walimu 15,919 na shilingi bilioni 27.15 kwa watumishi wasiokuwa walimu 11,470
- Madai yote yaliyoonekana kuwa sahihi ya shilingi bilioni 43.39 yatalipwa pamoja na mshahara wa mwezi Februari 2018 kwa mkupuo mmoja. Malipo ya Madai haya ambayo mengine yana zaidi ya miaka kumi majina ya walipwaji wote yatatangazwa kwenye magazeti kuanzia kesho tarehe 10 Februari, 2018.
Kwa matokeo hayo ya uhakiki, mazoezi yaliyofanyika likiwemo
zoezi la kuwaondoa kwenye Mfumo wa malipo ya mshahara (“payroll”)
watumishi hewa, vyeti feki na wasio kuwa na sifa na uhakiki wa madai ya malimbikizo ya
mishahara uliofanyika limeweza kuokoa jumla ya shilingi bilioni 84.22 ambazo ni sawa na asilimia 66 ya madai
yote ya malimbikizo ya awali ya shilingi bilioni 127.61 yaliyokuwa kwenye mfumo
ambazo bila zoezi la uhakiki kufanyika zingelipwa wakati zilikuwa hazistahili
kulipwa.
Serikali itaendelea kulipa madai ya watumishi kadiri yanavyojitokeza
ili kuondokana na malimbikizo ya aina hii ambayo yanaweza kuisababishia
Serikali hasara kwa kulipa madai yasiyostahili.
Asanteni kwa kunisikiliza