MKOPO WA DOLA MILIONI 65 WA KAGERA SUGAR WAWEKEZWA NCHINI

April 09, 2018

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, akijibu swali la Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, Bungeni Mjini Dodoma,  aliyetaka kujua sababu za Serikali kumdhamini mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Kagera, kukopa kiasi  cha dola milioni 65 za Marekani  ambacho amedai kimepelekwa kuwekezwa nchini Kongo  wakati Tanzania ina uhaba wa sukari.


Na Benny Mwaipaja

Serikali imeeleza kuwa kiasi chote cha dola za Marekani milioni 65 zilizokopwa na Kiwanda cha Sukari cha Kagera kutoka Benki ya CRDB kwa udhamini wa Serikali mwaka 2004 kimewekezwa nchini na hakijapelekwa kuwekeza katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa aliyetaka kujua sababu za Serikali kumdhamini mwekezaji wa Kiwanda hicho kukopa kiasi hicho cha fedha ambacho kimepelekwa kuwekezwa nchini Kongo wakati Tanzania ina uhaba wa sukari.

Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa uwekezaji uliofanywa katika Kiwanda cha Kagera ni wa takribani dola za Marekani milioni 250 hivyo haiwezekani mwekezaji kukopa dola milioni 65 na kuzipeleka Congo ili hali kiwango cha uwekezaji nchini ni kikubwa.

“Mwekezaji wa Kiwanda hicho ni wa ndani na amejitahidi kuajiri watanzania wengi hivyo Serikali ipo katika mchakato wa kukiwezesha kiwe cha mfano ili kiendelee kuleta matokeo chanya kwa watanzania”, alisema Dkt. Kijaji.

Katika swali la msingi la Mbunge huyo, alitaka kujua kiwango cha hisa ambacho Serikali inamiliki katika kiwanda cha Sukari cha Kagera na kiasi cha fedha kilichokopwa na kulipwa na mwekezaji huyo kupitia udhamini huo wa Serikali.

Dkt. Kijaji alieleza kuwa Serikali kwa sasa haimiliki hisa zozote katika kiwanda hicho na kuongeza kuwa hisa zake katika kiwanda hicho ziliuzwa mwaka 2001 baada ya kukibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni ya Kagera Saw Mills Limited.

Aidha Dkt. Kijaji alifafanua kuwa mwekezaji wa Kiwanda hicho alikopa kiasi cha dola za Maerekani milioni 65 kwa kutumia udhamini wa Serikali mwaka 2004, ikiwa ni udhamini (guarantee) wa kipindi cha miaka 12. Alisema kuwa mpaka sasa kiwanda hicho mimerejesha zaidi ya dola za Marekani milioni 56.88, sawa na asilimia 87.5 ya mkopo wote, na kwamba marejesho ya mkopo uliobaki wa Dola milioni 8.12 yatafikia ukomo wake mwezi Julai, 2019.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »