LIGI YA WANAWAKE KUANZA NA LIGI NDOGO

September 06, 2017
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeagiza Makatibu wa Vyama vya Mikoa kutuma haraka majina ya timu mabingwa wa mikoa wa soka la wanawake wa msimu wa 2016/17.

Viongozi wa mikoa wamekumbushwa kutuma timu ili kufanya maandilizi ya haraka ya Ligi Ndogo itakayofanyika Septemba 22 hadi 29, mwaka huu.

Ligi Hiyo ndogo inachezwa kutafuta timu mbili zitakazopanda daraja kucheza Ligi Kuu soka ya wanawake msimu wa 2017/2018.

Huu ni msimu wa pili wa ligi ya wanawake kwani msimu uliopita, timu shiriki zilikuwa 12 na Mlandizi Queens ya Pwani iliibuka bingwa wa kwanza katika historia ya soka hapa nchini.
Mara baada ya kumalizika kwa Ligi Ndogo, TFF itaanza taratibu za kupanga kuanza kwa Ligi Kuu kwani wakati huo tayari tutafahamu timu ambazo zimepanda. Ligi Ndogo haitahusisha timu ambazo zimecheza Ligi Kuu msimu wa 2016/17.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »