Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla
amewataka viongozi wa Serikali na wale wenye upande wa mgogoro wa pori tengefu
la Loliondo kukaa chini ili kupata ufumbuzi wa suala hilo lililochukua karibu
miaka zaidi ya 20 sasa huku akitoa tamko la kusitisha operesheni zote
zilizokuwa zikiendelea katika suala hilo.
Waziri Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo kwenye mkutano wa
wazi jioni ya jana Oktoba 26,2017 wakati akizungumza mamia ya wananchi wa
Loliondo wakiwemo wale wenye mgogoro na pori hilo.
“Kuanzia leo, mimi kama Waziri wa Maliasili na Utalii, nina
waahidi kufanya uhifadhi endelevu, kukaa na wananchi kuhifadhi. Hivyo nawaomba
viongozi wa Serikali na wananchi kwenye mgogoro huu sasa kufikia mwisho na
kukaa meza moja.
Mgogoro utatatuliwa kwa kukaa mezani. Kwa pande zote mbili
sasa kuja na jibu moja juu ya kusitisha mgogoro huu. Hatutaki tumuone Mkuu wa
Wilaya mbaya ama Mkurugenzi wake ama wahifadhi wabaya au Waziri wa
Maliasili bali, sote tuwe kitu kimoja
katika meza ya majadiliano na kufikia mwisho” alieleza Dk.Kigwangalla.
Ameongeza kuwa:
“Tutasimamia kushirikiana na nyie. Lakini hatutokubalana na
watu miongoni mwetu wa watu ambao wataivunja sheria kwa makusudi. Kwa msingi
huo, napenda kutamka kuwa, nasitisha operesheni iliyokuwa ikiendelea Loliondo
ile ya kukamata wafugaji na kuwatesa ama vitendo vingine vibaya.
Pili naagiza watalaam wa maji, wakae na watalaam wa hifadhi
washirikiane na serikali ya kijiji wawaruhusu wafugaji kunywesha mifugo yao.
Pia naagiza kwa Wahifadhi na Kamati ya Ulinzi na Usalama,
mifugo yote ambayo imekamatwa na mamlaka ambayo ipo chini ya Wizara ambayo
nasimamia mimi ile yote ambayo haijahukumiwa na mamlaka za kisheria iachiwe
huru kwa wenyewe kwa mifugo ambayo itabaki chini ya idara iliyopo
kwenye wizara yangu ni ile yenye migogoro ya usuluhishi tu” alieleza
Dkt.Kigwangalla.
Waziri Dkt.Kigwangalla yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya siku
sita ambapo awali alianza kutembelea Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)mjini
Arusha, na baadae Mamlaa ya Hifadhi ya Ngorongoro ambapo pia aliweza kukutana
na jamii ya wafugaji wanaoishi kwenye hifadhi ya Ngorongoro kwa namna ya
kitatua migogoro kati yao na wahifadhi wa Ngorongoro.