(Picha na Benedict Liwenga-Maelezo)
………………………………………………………………………………………
Na. Lilian Lundo – Maelezo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki
amemsimamisha kazi aliyekuwa mkuu wa chuo cha Utumishi wa Umma Said
Nassoro kutokana na kushindwa kusimamia watumishi walioko chini yake
Mhe. Kairuki ametoa maamuzi hayo
leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari katika
moja ya kumbi zilizopo katika ofisi za Utumishi wa Umma.
“Namsimamisha Bwana Said Nassoro
aliyekuwa mkuu wa chuo hiki kwa kushindwa kusimamia watumishi walioko
chini yake na kupelekea suala zima la usimamizi wa shughuli za chuo
hususani katika matawi yake mbalimbali yaliyoko mikoani kuathirika,”
alisema Mhe. Kairuki.
Mhe. Kairuki aliongeza kwa kusema
kuwa usimamizi wa Bw. Nassoro ambao haukuwa wa ufanisi umetoa mwanya
kwa viongozi mbalimbali wa matawi kufanya ubadhilifu wa mali za Umma
ambapo mwaka 2011 na 2013 aliyekuwa mkurugenzi wa chuo upande wa tawi
la Mtwara Silvanus Ngata aliongeza gharama za ujenzi.
Aidha taarifa kutoka Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na TAKUKURU zilithibitisha
ubadhilifu huo lakini mkuu huyo wa chuo hakuweza kuchukua hatua yoyote
badala yake alimuhamisha Bw. Ngata kwenda kwenye tawi la Tabora na
kuendelea na wadhifa wake.
Kutokana na ubadhilifu huo
imempelekea Mhe. Kairuki kumsimamisha kazi Bw. Ngata ambaye alikuwa
Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Tabora na Bw. Joseph
Mbwiro kutokana na matumizi mabaya ya fedha za malipo ya ada kiasi cha
shilingi bilioni moja ambazo zilikuwa zikilipwa na wanafunzi kwa mwaka
wa fedha 2014/15.
Mhe. Kairuki ameendelea kueleza
kuwa bado wanaendelea kuondoa watumishi wa Umma ambao hawafuati
mifumo na miongozo ya Utumishi wa Umma ili kuwabakiza watumishi ambao
wanaonyeshe taswira nzuri na kufuata mifumo na miongozo ya Utumishi wa
Umma kwa ukamilifu wake.
EmoticonEmoticon