MWENYEKITI WA UVCCM MKOA WA TANGA AJITOSA UBUNGE JIMBO LA KOROGWE MJINI.

July 24, 2015
KULIA NI MWENYEKITI WA JUMUIYA YA UMOJA WA VIJANA MKOA WA TANGA(UVCCM)ABDI MAKANGE AKIKABIDHIWA FOMU ZA KUOMBA KUTEULIWA NA CCM KUWANIA UBUNGE JIMBO LA KOROGWE MJINI








MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Tanga, Abdi Makange juzi alichukua fomu za kuomba kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania Ubunge Jimbo la Korogwe mjini katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Octoba mwaka huu hapa nchini.

Makange anakuwa ni kada wa kumi na tatu wa chama hicho kujitokeza kuomba ridhaa hiyo huku wengine Allen Nyangasa,Proffesa Catherbet Mhiliu,Kanali Iddi Kipingu,Salma Mntambo,Mussa Bareko,Yusuph Abdallah Nassir,William Mgaza.

Wengine ambao waliokwisha kujitokeza kutaka nafasi hiyo kupitia (CCM) ni Deogratius Augustino, Marry Chatanda, Thobias Mugweta,Seif Abdallah Shekalage,Fransis Shalimbago na Mjata Daffa Abdallah.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi mara baada ya kuchukua fomu hizo, Makange alisema kuwa dhamira yake ya kuwania nafasi hiyo ni kutaka kuhakikisha jimbo hilo linapata maendeleo ndani kipindi chake cha miaka mitano katika sekta mbalimbali ikiwemo huduma za Afya, Miundombinu na huduma za upatikanaji maji ya uhakika kwa wakazi.

Alisema kuwa katika kipindi ambacho ataliongoza jimbo hilo endapo atapewa ridhaa na wananchi hao atahakikisha anaweka mipango mizuri itakayopelekea kwenye Jimbo hilo kuwa na hospitali ya wilaya ili kuipunguzia mzigo ile ya Magunga ambayo wananchi kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo na nje wanakwenda kupata matibabu.

Aidha alisema kuwa suala la wakina mama ambao wanajifungulia kwenye mifuko ya rambo kutokana na ukosefu wa vifaa atahakikisha analivalia njuga jambo hilo kwa kuboresha vifaa tiba kwenye hospitali na vituo vya afya vilivyopo kwenye Jimbo hilo ili kuondoa adha kwa wakinamama ambao wamekuwa wakipata matibabu kwenye hospitali wilayani humo.

   “Hili ni tatizo kubwa sana hivyo nisema tu suala hili nitahakikisha
ninalipa kipaumbele kikubwa sana wakati nitakapokuwa mbunge wenu kwa kuweka mipango imara itakayoleta ufanisi na hatimaye kuweza kuondoa kabisa “Alisema Makange.

Alisisitiza katika suala la Afya akiwa kama mbunge atatilia mkazo
wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo yeye
atachangia asilimia 10 ya mshahara wake kuwalipia ili kuweza kupata matibabu wakati wote wanapokuwa wakiugua jambo ambalo litasaidia kuendeleza huduma za afya.

Akizungumzia suala la miundombinu, Makange alisema kuwa katika Jimbo hilo zipo baadhi ya barabara hazina hadhi ya mji huo kutokana na nyingi kuwa za changarawe hivyo atahakikisha analifanyia kazi suala hilo kwa kuweka lami ili mji huo kuwa na muonekana mzuri.

Kwa upande wa huduma za upatikanaji wa maji,Makange alisema kuwa suala hilo atalivalia kibwebwe kwa kutumia vizuri mto Ruvu kupitia wahisani ili kutoa maji kwenye mto huo ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi kwenye Jimbo hilo sambamba na kuchimba visima kwenye baadhi ya maeneo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »