WILAYA YA MUHEZA YAANZA JITIHADA ZA KUKABILIANA NA TATIZO LA MAJI.

May 05, 2014
NA OSCAR ASSENGA, MUHEZA.

WILAYA ya Muheza imeanza kuchukua jitihada mbalimbali za kukabiliana na tatizo la maji Muheza mjini hapa ikiwemo kuchimba kisima cha Polisi Mangenya na kuendeleza kisima cha kitisa kilichokuwa kinatumiwa na mamlaka ya Mkonge.

Mkuu wa wilaya hiyo, Subira Mgalu aliyasema hayo hivi karibuni ambapo alisema visima virefu tisa vimechimbwa maeneo ya Muheza mjini, Lusanga na Kitisa vyote vina uwezo wa kutoa maji.

Mgalu alisema utaratibu wa upimaji wa ubora wa maji umeandaliwa ili maji hayo yaanze kutumika ambapo mradi huo ulijengwa mwaka 2013 na chanzo chake ni kisima kirefu chenye kina cha mita 57 na uwezo wake ni lita 5000 kwa saa.

Alisema kisima hicho kilichimbwa na wizara ya mambo ya ndani mnamo mwaka 1998 na baadaye kuhujumiwa na watu wasiojulikana ambapo mwaka 2010 kisima hicho kilisafishwa kwa jitihada za halmashauri ya wilaya ya Muheza na kujengewa chemba yenye mfuniko na kufuli.

Aliongeza kuwa kutokana na kero kubwa iliyopo katika wilaya ya Muheza mjini ilipatikana fedha kutoka wizara ya maji mnano jaunari 2013 jumla y ash.milioni 100. kwa ajili ya kuendeleza kusima cha Polisi.

Mradi huo umekamilika na unatoa huduma kwa wananchi wa muheza mjini hususani katika eneo la genge ya zamani,kituo cha polisi na shule ya sekondari Chifu Mangenya.

Katika hatua nyengine, Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Muheza,Hans Patrick  alisema kiasi cha sh.bilioni 13.4 zinahitaji ili kuweza kutatua kero ya maji wilaya ya Muheza mjini kutokana na huduma kutokuwa ya uhakika hali ambayo inapelekea baadhi ya wananchi kutafuta huduma hiyo umbali mrefu.

Patrick alisema kuwa gharama hizo zitatumika kwa ajili ya kutoa maji mto zigi kwa ajili ya kusambaza maeneo yote yaliyopo mijini ambayo yanakabiliwa na changamoto ya kutokupatikana maji kwa uhakika

Alisema hivi sasa wanajitahidi kutafuta wafadhili mbalimbali ambao wataunganisha nguvu zao na fedha kutoka serikalini ili kuweza kuanza mradi huo ambao utakuwa ni mkubwa yenye lengo la kuondoa kero ya maji kwenye wilaya hiyo ambayo imekuwa kubwa.

Mhandisi huyo alisema mradi huo tayari ulishapata baraka kutoka wizara husika ambao awali walishapelekea mhandisi mshauri kwa ajili ya kwenda kuuangalia ambapo utakapokamilika utahudumia wakazi wa vijiji vya Kisongeni, Kisiwa Ngumba na Mto zigi.

Alieleza kuwa wananchi wa Misongeni, Ubembe,Mikwamba,Kwemhosi,Masimbani na Mamboleo wanapata maji yam to mgobe ambao mradi wake ulitumia kiasi cha sh.milioni 839 na tayari ulishakamilika ikiwemo kuanza kazi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »