Viongozi wa
vijiji vya Bombo majimoto, Bombo Mtoni,Kijungumoto na Kwetonge vilivyopo kata
ya Mashewa wamelalamikiwa kukosa uzalendo na kutuhumiwa kushirikiana na
raia
wanaosadikiwa kutoka nchi jirani ya
Kenya kuvuna msitu wa asili wa miti ya Mkarambati unaozunguka vijiji hivyo kwa
ajili ya kuchongea vinyago ambavyo huuzwa kwa Watalii nchini Kenya.
Hayo
yamebainishwa juzi na baadhi ya Wananchi wa vijiji hivyo waliokutwa katika
msitu huo wakikusanya kuni wakati wa operesheni maalum iliyolenga kuwakamata
waharibifu wa msitu huo ambayo iliendeshwa na kamati ya ulinzi na Usalama ya
wilaya ya Korogwe kwa kushirikiana na wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS)
na Halmashauri ya wilaya ya Korogwe.
Akizungumza
na kamati ya ulinzi na usalama mkazi wa Bombo majimoto Shaban Said alisema kuwa
mara nyingi wameshajaribu kutoa taarifa kuhusu uhalifu unaoendelea katika msitu
huo ngazi ya kijiji lakini wamekuwa wakidhihakiwa kuwa wana vyeo gani
serikalini hata walisemee suala hilo na hivyo imekuwa ngumu kwao kama Wananchi
kukomesha ujangili huo wa msitu.
“Ili
mhakikishe kuwa wanashirikiana ndiyo maana hata hawatembelei msitu mara kwa
mara kwani wangeshachukua hatua kabla ya nyie kuja kutokana na uharibifu mkubwa
uliofanyika humu ndani ya msitu, lakini sisi tukipeleka taarifa tunaulizwa tuna
vyeo gani.” Alisema Said.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mashewa
inayozungukwa na msitu huo Seif Hillaly,
alisema yeye binafsi na uongozi wa kata walishafanya doria katika msitu
huo na kufanikiwa kuwakamata wahalifu
lakini hata hivyo waliachiwa huru baada
ya kulipa faini kulingana na sheria za
nchi,hivyo alitoa rai kwa watunga Sheria
kutunga Sheria kali zenye adhabu itakayowatofautisha wazawa na wageni ili
kukomesha kabisa tabia ya raia wa nchi nyingine kuingia Tanzania na kuharibu
misitu.
Mkuu wa
wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wanafanya juhudi kama
Serikali kwa ushirikiano na idara ya uhamiaji kuwatia nguvuni watu hao
wanaosadikiwa kuingia nchini kinyemela na kufamya uhalifu huo na kwamba
atatumia vyombo vya dola kuchunguza na kuwabaini viongozi wanaoshirikiana
nao,pia alitoa wito kwa Watanzania kuwa
Wazalendo na kulinda nchi yao wao wenyewe kwani msitu huo unawafaidisha
Watanzania hivyo kuathirika kwake ni hasara kwa Watanzania huku wakenya
wakibaki salama na nchi yao.
Awali akitoa
taswira ya uharibifu wa msitu huo, Afisa Misitu Msaidizi wa TFS Mbwelwa Kimweri
alisema msitu huo wenye ukubwa wa hekta 3500 umekwishaharibiwa kwa asilimia 90
na sababu kubwa ikiwa ni ukosefu wa uzalendo kwani TFS na Halmashauri
wameshatoa elimu ya kutosha kwa wanajamii hao kuhusu umuhimu wa msitu huo na
jinsi ya kuuhifadhi huku wakiendelea kufaidika nao.
Operesheni
hiyo ilifanikisha kukamatwa kwa mtu mmoja anayedhaniwa kuwa raia wa Kenya ambaye alifikishwa katika kituo
cha polisi wilayani Korogwe na hatua za awali za kufunguliwa mashtaka
zimekwishafanyika.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ikijipanga katika makundi kuingia Msituni kusaka waharibifu wa Msitu. |
Safari kuelekea Msituni |
Kikosi kazi kilipovamia kambi ya Majangili hao wa Msitu na kukuta wametoroka,hata hivyo kikosi hicho kilimpata mmoja wao ambaye anashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani Korogwe |
Mgambo wakitoka na Shehena ya vinyago Msituni vilivyokuwa vikiendelea na matengenezo kabla ya msitu kuvamiwa na Kamati ya Ulinzi. |
EmoticonEmoticon