SIMBA SC YAZINDUKA,YAWAFUMUA RUVU SHOOTING 3-2, TAMBWE APIGA MBILI

March 02, 2014
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
SIMBA SC imezinduka baada ya jioni hii kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliochezwa sambamba na mvua mwanzo hadi mwisho, hadi mapumziko tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Mrundi Amisi Tambwe aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya 25 baada ya kuwahi mpira uliotemwa na kipa Abdallah Rashid kufuatia shuti la mpira wa adhabu la Said Ndemla.
Mtambo wa mabao; Amisi Tambwe akishangilia baada ya kufungfa bao la pili leo
Jonas Mkude akimpongeza Tambwe baada ya kufunga

Tambwe tena alifunga bao lake la 19 msimu huu wa Ligi Kuu dakika ya 33 akiunganisha krosi ya Nahodha Haruna Shamte kutoka kulia.
Kipindi cha pili, Ruvu Shooting inayofundishwa na Mkenya Thom Olaba, ilibadilika kidogo na kufanikiwa kupata bao dakika ya 74, mfungaji Said Dilunga aliyemalizia kona ya Michael Aidan Pius.
Hata hivyo, winga wa Simba SC, Haroun Athumani Chanongo aliifungia timu yake bao la tatu dakika ya 76 baada ya kupata pasi nzuri kutoka kwa Amri Kiemba.
Shambulizi la kushitukiza la Ruvu lilisababisha kizazaa na piga nikupige langoni mwa Simba SC na beki Joseph Owino akaunawa mpira, refa Nathan Lazaro wa Kilimanjaro akamezea, lakini Ramadhani Singano ‘Messi’ akaunawa tena na mwamuzi huyo akatenga tuta, lililokwamishwa nyavuni na Jerome Lambele dakika ya 82. 
Ushindi huo, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 35 baada ya kucheza mechi 19 na kuendelea kubaki nafasi ya nne  nyuma ya Mbeya City yenye pointi 36, Yanga pointi 38 na Azam FC pointi 40 kileleni.
Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Yaw Berko, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Haroun Chanongo, Said Ndemla/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk82, Amisi Tambwe/Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ dk78, Amri Kiemba na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Michael Pius, Mao Bofu, Baraka Jafari, Gedion Sepo, Ali Khan, Hamisi Kisuke/Ayoub Kitala dk46, Juma Nade/Juma Mdindi dk40, Elias Maguri/Jerome Lambele dk61, Said Dilunga na Raphael Kyala.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »