March 12, 2014

Megawati 150 kuongezeka katika Gridi ya Taifa

1 (3)Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji Mhandisi Decklan  Mhaiki (katikati) akimweleza Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo  (kushoto) pamoja na Waandishi wa habari moja ya mashine za kufua Umeme zitakazofungwa katika  eneo la Kinyerezi I jijini, Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Mradi wa ujenzi huo, Bw. Shaun Moore.
2 (1)Mmoja wa mitambo ya kufua umeme ambao utafungwa katika eneo la Kinyerezi I mara baada ya ujenzi kukamilika. Mitambo hiyo, inatarajiwa kuzalisha kiasi cha megawati za umeme 150 ambazo zitaunganishwa katika gridi ya Taifa.

3 (2)Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo katika picha ya pamoja na baadhi ya watendaji kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini na watumishi wa kampuni inayojenga kituo hicho ya Jacobsen Elektro.  
4 (2)Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa Mradi wa ujenzi wa kituo cha Kinyerezi I, Bw. Shaun Moore, wakati akimweleza maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
……………………………………………………………………………………..
Na Asteria Muhozya na Jema Marko, Dar es Salaam
Megawati 150 zinatarajiwa kuongezeka katika gridi ya Taifa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme eneo la Kinyerezi I pamoja na kukamilika kwa ufungaji wa mitambo hiyo, ambapo shughuli zima inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Disemba mwaka 2014.
Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo  hicho  alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa  kituo hicho  ni  hatua  mojawapo ya kutimiza azma  ya Serikali ya kuongeza umeme katika gridi ya Taifa.
Aidha, aliwataka watanzania na wateja wa umeme kujenga imani na Shirika la Umeme Tanzania kutokana na mabadiliko ambayo tayari yamefanyika katika shirika hilo ikiwemo utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika.
“Nataka Watanzania muelewe kuwa, Tanesco ya sasa sio kama ya zamani. Umeme utapatikana. Kampuni ya Jacobsen Elektro ambao wanafanya kazi ya ujenzi ni wazoefu katika shughuli hizi, tuna imani kazi itakwenda vizuri kama tulivyopanga. Tanesco itatatua tatizo la umeme”. Alisema Waziri Muhongo.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo   alieleza kuwa, asilimia 98 ya kampuni za kitanzania kupata   kandarasi katika ujenzi huo ni fursa mojawapo ambazo watanzania wanatakiwa kuzitumia katika kipindi hiki ambacho nchi inaingia katika uchumi wa gesi.
Akizungumzia kuhusu fedha za ujenzi wa kituo cha kinyerezi I na ujenzi wa vituo vingine vya kinyerezi II, III na IV, Waziri Sospter Muhongo alieleza kuwa,  fedha  za ujenzi wa kituo cha Kinyerezi I zimetolewa na Serikali kupitia TANESCO.  Ujenzi wa kituo cha kinyerezi II fedha itatokana  na ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Japani , wakati ujenzi wa kinyerezi III na IV fedha zitatokana na kuingia ubia kati ya Serikali  na kampuni ya Kichina.
Wakati huo huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji, wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Decklan Mhaiki, aliongeza kuwa, katika kituo hicho zitafungwa jenereta nne ambapo kila moja itakuwa na uwezo wa kuzalisha kiasi cha megawati 37.5, hivyo kufanya jumla ya megawati 150 kutoka kituo hicho.
Vilevile, alieleza kuwa, katika jitihada za kuhakikisha kwamba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linatatua tatizo la Umeme nchini, tayari shirika hilo na mkandarasi anayejenga kituo hicho, kampuni ya Jacobsen Elektro wameanza mazungumzo ili kuongeza kiasi kingine cha megawati 200 ili kituo cha kinyerezi I kiweze kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 350.
Akielezea kuhusu ubora wa jenereta zitakazofungwa kituoni hapo, Mhaiki alieleza kuwa, generator hizo ni za kisasa na hazina athari za kimazingira ikiwemo kelele.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Jacobsen Elektro, Bw.  Shaun Moore, akielezea maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, alieleza kuwa, ujenzi wa kituo hicho unaendelea vizuri kutokana na kampuni hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano mzuri na kampuni za kitanzania zilizochukua kandarasi tofauti tofauti za ujenzi wa kituo hicho, ambapo takriban asilimia 98 ya kandarasi  na wafanyakazi ni kutoka  kampuni za kitanzania.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »