SERIKALI YATAKIWA KUTOA KODI KATIKA NYUMBA ZA (NHC).

February 17, 2014
Na Khadija Baragsha, Mkinga.

KAMATI ya  kudumu ya Bunge ya  Ardhi, Maliasiri na Mazingira  imeitaka serikali kuondoa kodi  kwenye vifaa vya  mradi wa ujenzi wa nyumba za  gharama  nafuu unaoendeshwa na Shirika la Nyumba Tanzania (NHC)  ili kumuwezesha mwananchi wa hali ya chini kuondokana na makazi duni.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jemes  Lembeli aliyasema hayo baada ya  taarifa ya mradi huo iliyosomwa mbele ya kamati hiyo na Mkurugenzi wake, Benedict  Kilimba na kueleza kuwa kodi za serikali zimesababisha  bei ya nyumba hizo kuwa kubwa.


Kwamujibu wa taarifa ya meneja huyo ni kwamba  mfumo  wa kuwataka  wanunue  vifaa vya ujenzi  kwenye maduka maalumu kumeongeza  gharama ya ujenzi huo  na kufikia tsh mil, 31.3 kwa nyumba  yenye vyumba viwili na tsh mil, 35.3 hadi tsh mil, 36.2 kwa vyumba vitatu  bila VAT.


Kilimba alidai kuwa  mbali na changamoto hizo  shirika pia linalazimika kuilipa serikali kiasi cha tsh mil, 7 mpaka tsh mil, 10  kama kodi  ya ongezeko la thamani VAT   kutokana  na  manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa kila nyumba jambo lililosababisha nyumba hizo kuuzwa  tsh mili, 40. 7  kwa  nyumba ya vyumba viwili na tsh million 46. 3 hadi  tsh mil, 48.2  kwa vyumba vitatu.


Hata hivyo  alieleza kuwa  kama shirika litaruhusiwa kutafuta maduka yenye unafuu na  serikali ikaondoa  kodi ya VAT  mauzo ya nyumba hizo yangeweza kufikia tsh mili, 28  bei ambayo mtu wa hali ya chini angeweza kuimudu tofauti na ilivyo  sasa


Akizungumza baada ya taarifa hiyo, Lembeli alisema ni wajibu sasa kwa serikali kuonyesha moyo wa dhati katika kuwawezesha wananchi kumudu kubadilisha maisha yao ikiwemo hili la makazi bora ambayo ni haki ya kila mtu.


Aliahidi kubeba jukumu la kuishauri serikali kuondoa kodi ya VAT  kwenye  vifaa vya ujenzi wa nyumba zinazojengwa na mradi wa shirika hilo hasa zile zilizolengwa kwa ajili ya  makazi bora kwa watu wa hali ya chini.


“Sisi wanakamati tumetembea katika nchi mbalimbali kama vile nchi ya Singopore, tumejionea na  kujifunza jinsi serikali ya nchi hiyo inavyowawezesha watu wake katika makazi bora……..takriban asilimia 90 ya nyumba zilizojengwa na serikali ya nchi hiyo zimeuzwa kwa wananchi kwa bei nafuu, vipi sisi huku!” alihoji Lembeli.


Hata hivyo alidai kuwa taarifa ya shirika hilo kuhusu mazingira ya ujenzi wa nyumba hizo inaonyesha kwamba mtu wa kawaida hatakuwa na uwezo wa kuzinunua kutokana na ukubwa wa bei jambo alilolieleza kuwa linaondoa maana halisi ya azma iliyokusudiwa na serikali yenyewe ama wananchi walalahoi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »