KOCHA AHLY AGOMA KUJIUZULU ,AISUBIRI YANGA.
KOCHA Mkuu wa Al Ahly ya Misri, Mohammed Youssef, ameziba
masikio na kutupilia mbali kelele za mashabiki wanaomshinikiza ajiuzulu
kutokana na matokeo mabaya na kesho Jumatano anaiingiza timu kambini.
Ahly inajiandaa na msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa
ambapo itaanza na Yanga mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam,
lakini kesho kutwa Alhamisi itacheza mechi ya ‘Super Cup’ dhidi ya
Safaxien ya Tunisia nchini Misri kwenye Uwanja wa Cairo.
Mechi hiyo ni kuashiria mwanzo wa msimu mpya wa
mashindano ya kimataifa na hukutanisha bingwa wa Kombe la Shirikisho na
wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Mashabiki wa Al Ahly wanahofia kwamba mwenendo wa
timu hiyo katika ligi yao ya ndani usije ukaiathiri na kukumbana na
kipigo cha aibu kutoka kwa Yanga na wakaondoshwa mapema na kuwa timu ya
pili ya Misri kuondoshwa mashindanoni na timu ya Tanzania ikiwa bingwa
mtetezi. Simba iliitoa Zamalek mwaka 2003 wakati Wamisri hao wakiwa
mabingwa watetezi.
Kocha huyo alisema kwamba kujiuzulu siyo hoja ya
msingi kwa sasa kwa vile timu hiyo inayumba kutokana na majeruhi
waliomo, ingawa kocha wa Yanga, Hans Pluijm, amedai hiyo ni danganya
toto tu ili wajisahau.
Akizungumza baada ya mchezo wao wa mwisho
uliopigwa wikiendi iliyopita dhidi ya vibonde katika kundi lao El
Gounah ambapo Al Ahly ilipokea kipigo cha bao 1-0, Youssef alisema
licha ya kikosi chake kupokea kipigo cha tatu tangu kuanza kwa ligi
hiyo, matokeo ambayo yaliwashusha mpaka nafasi ya tatu, hana mpango wa
kuachia ngazi.
Youssef alisema kwa sasa kikosi chake kinapita
katika wakati mgumu na wanasumbuliwa na tatizo la majeruhi ambao ni
kiungo mshambuliaji, Walid Soliman na mabeki wao wa pembeni; Ahmed Fathi
na Sayed Moawad.
Alisema bado timu yake ina nafasi ya kurudisha
makali yao ambapo amewataka wachezaji wake kusahau matokeo ya mchezo huo
haraka na kujikita katika kuangalia michezo ya Ligi ya Mabingwa.
“Sina mpango wa kujiuzulu kwa sasa, nitabaki
kuondoa changamoto tunazokutana nazo kwa sasa, nataka wachezaji wangu
kusahau kila kitu kuhusu kufungwa kwetu katika mchezo uliopita,
nawaamini wachezaji wangu wanao uwezo mkubwa wa kuirudisha timu katika
mwendo mzuri,” alisema Youssef.
“Najua kwamba kuna presha kubwa kwa wachezaji
wangu hasa katika hiki kipindi kigumu ambacho tunachopitia, tuhahitaji
kupewa muda kuwa sawa, huu ni mchezo wa soka lolote linaweza kutokea
wakati wowote.”
Yanga itamtuma kocha msaidizi wake, Boniface Mkwasa, kwenda Cairo kuiangalia mechi hiyo ya Super Cup.
-mwanaspoti
-mwanaspoti